Habari za Punde

Wanajamii na Watendaji Kubadilika na Kuchukua Hatua za Ziada katika Kupambana na Uhalifu Unaojitokeza

 Na. Mwandishi OMKR

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amewataka wanajamii na watendaji mbali mbali kubadilika na kuchukua hatua za ziada katika kupambana na uhalifu unaojitokeza katika maeneo mbali mbali nchini.

Mhe. Othman ameyasema hayo alipofika kuifariji  Familia ya Mfanyabiashara maarufu nchini Said Salim Bakharesa kufuatia kifo cha mwanafamilia Salim Ahmed Salim Bakharesa, ambaye  alivamiwa na kujeruhiwa kwa visu na watu wasiojulikana na kusababisha kifo akiwa hopitalini nchi Afrika ya kusini  alikopelekwa kwa matibabu.

Mhe. Othman amesema kwamba watendaji wa vyombo mbali mbali hawanabudi kutambua kwamba mji wa Zanzibar umekua na tabia na miendo ya watu kubadilika sana na kwamba lazima wachukue hatua sahihi na za zaidi kutokana na mabadiliko hayo yaliyopo.

Amesema uhalifu unaojitokeza katika maeneo mbali mbali unatokana na kubadilika kwa tabia za wanajamii sambamba na kuongezeka watu wenye hulka tofauti jambo linalochangia kujitokeza vitendo vingi vya uhalifu hapa nchini.

Amesema kwamba wanajamii na wasimamizi wa  sheria nchini wanahitaji kuwa na mtazamo mwengine na kubadilika katika utendaji wa kazi zao na kuyatazama masuala mbali mbali kiutendaji kwa upana zaidi kuliko ilivyo sasa ili kukabiliana nayo kwa usahihi na uhakika.

Amesema kwamba tabia mseto zinazojitokeza Zanzibar zinachangia sana kuwepo matukio ya aina mbali mbali ya uhalifu jambo linalohitaji watendaji kufanya kazi ya ziada katika kupambana na hali hiyo isiendelee nchini.

Amefahamisha kwamba jamii na vyombo mbali mbali vya utendaji vinahitaji kufanya marekebisho ya utendaji wao ili kuwa na mbinu bora na za kisasa katika kukabiliana na uhalifu wa aina mbali  mbali nchini.

Amefahamisha kwamba  licha ya serikali kujitahidi  kuweka mikakati imara  katika kupambana na masuala mbali mbali yakiwemo ya uhalifu na hasa udhalilishaji, lakini masuala  hayo yamekuwa yakiongezeka  kutoka na mji kukua na  idadi ya watu kuongezeka na kwamba mabadiliko ya kiutendaji ni jambo linalohitajika sana katika maeneo yote.

Mhe. Othman aliitaka familia  hiyo kuendelea kuwa na subra na ustahamilifu katika kipindi kigumu cha msiba wa kuondokewa na mwanafamilia wao na kuendelea muombea dua marehemu ili kupata msamaha wa mola muumba.

Naye mwanafamilia hiyo Ahmed Salim Bakharesa amesema kwamba kuna haja kubwa kwa serikali kufikiria kuweka mkazo na kuipa nguvu zaidi poliisi jamii ili isaidie vyema katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu wa aina mbali mbali nchini.

Marehemu Salim Ahmed Salim Bakharesa, aliyevamiwa na watu wasiojulika nyumbani kwake na kujeruhuiwa kwa kisu wiki chache  zilizopita alipelekwa kwatika Hospitali Hill Park Mjini Johanasbag Afrika kusini ambako alifariki na kuzikwa jana .

 Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kupitia Kitengo chake cha Habari leo tarehe 29.12.2022.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.