Na. Maulid Yussuf -- Zanzibar
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Bi.Abeida Rashid Abdalla amewataka watendaji kutoka Taasisi mbali mbali za Serikali kutoa maoni yao yatakayosaidia kuimarisha mpango kazi wa Kitaifa wa wanawake amani na usalama.
Akifungua mkutano wa wadau wa kupokea maoni ya uboreshaji wa rasimu ya mpango kazi huo uliofanyika katika ukumbi wa Zanzibar Beach resort Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar bi Abeida amewataka washiriki hao kuangalia kila Taasisi na Idara kuwa kuna kitu gani ambacho wanaweza kuingiza kwenye mpango kazi kwa lengo kuwezesha utekelezaji wake.
Aidha amewataka kuangalia masuala ya faraja na ahuweni, kwa kuwa ni eneo ambalo halijashughulikiwa katika kiwango cha kutosha katika rasimu ya mpango kazi.
Pia amesema bado kuna nafasi ya kutoa maoni katika njia ya maandishi na kupeleka sehemu husika na kuwataka wadau hao kufanya vikao kama hivyo kwa upande wa Pemba kwani itaisaidia kuongeza ushiriki, umililiki na uwelewa.
Nae Mwakilishi Mkaazi wa UN Women Tanzania Ms Hodan Addou, amesema Tanzania ni nchi ya Amani na haina vita ila imezungukwa na nchi ambazo zina vita, hivyo kuwepo kwa mpango kazi huo kutaongeza na kuchangia juhudi za Serikali za kuhakikisha usawa wa kijinsia na ushiriki wa wanawake katika masuala ya uongozi, ulinzi na usalama katika vyombo vya maamuzi.
Ms Hoddan amepongeza juhudi za Serikali zote mbili chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar Dkt Hussein Ali Mwinyi za kuwezesha usawa wa kijinsia na ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali hasa za uongozi.
Mpango kazi huu ni utekelezaji wa maamuzi namba 1325 ya Baraza kuu la usalama la Umoja wa Mataifa ambalo limetaka nchi wanachama kuwa na mpango kazi wa aina hiyo ambapo Tanzania imeridhia maamuzi hayo.
mwisho
IMEANDALIWA NA KITENGO CHA UHUSIANO WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII JINSIA WAZEE NA WATOTO.
No comments:
Post a Comment