Habari za Punde

Wasiokagua Miradi Kuchukuliwa Hatua za Kinidhamu

Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Iramba Magharibi Mkoani Singida, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, akihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Ndago, ambapo pamoja na mambo mengine, aliwataka wananchi kubainisha maeneo yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji.

Na. Peter Haule, Singida

Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Iramba Magharibi, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amesema hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa wakaguzi wa ndani kuanzia ngazi ya Halmashauri hadi Wizara watakaoshindwa kukagua miradi ya maendeleo iliyokatika maeneo yao kwa wakati kwa sababu Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi lakini miradi mingi hailingani na fedha zilizotolewa.

Dkt. Nchemba ametoa maagizo hayo wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika  katika tarafa ya Ndago Wilayani Iramba mkoani Singida.

Alisema kuwa Mkaguzi kwenye Halmashauri za Wilaya hadi Wizara ambaye atasubiri miradi ikamilike kwenye eneo lake bila kufanyiwa ukaguzi na kusababisha makosa kubainishwa na mkaguzi wa nje kutoka makao makuu katika hatua za mwisho za mradi, atakuwa amejifukuzisha kazi.

“Eneo lolote ambalo miradi inaendelea kutekelezwa, nitaongea na wenyeviti wa Halmashauri na wabunge wote na mkaguzi wa nje akikuta eneo la mradi analoenda kukagua na mkaguzi wa ndani hajakagua, mkaguzi wa eneo lile atakuwa amejifukuzisha kazi mwenyewe”, alisema Dkt. Nchemba.

Dkt Nchemba alisema kuwa kumejengeka utaratibu kwa baadhi ya watumishi wa umma wakiisha ajiriwa wanafaidi mshahara na hawezi kufanya kazi bila posho licha ya kuwa maeneo ya ukaguzi yapo kwenye maeneo yao ya kazi na wameajiriwa kwa kazi hizo.

Alisema inashangaza kuona kuwa kuna eneo lina wahandisi zaidi ya watatu na wanalipwa mishahara kila mwezi bila kufanya ukaguzi wa miradi na matokeo yake wananchi wanajitoleaa kujenga majengo ili watoto waende shule bila kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wataalamu hao.

“Mwananchi anajenga jengo kuanzia hatua ya awali hadi anamaliza ndipo anatokea mkaguzi na kueleza kuwa kwa jinsi ninavyoona hili jengo halifai, alikuwa wapi kuanzia wanaweka tofali la kwanza hadi mwisho” alisema Dkt. Nchemba.

Alisema ameongea na Waziri wa TAMISEMI na kukubaliana kuwa mazingira hayo ya kutowajibika yatasababisha jengo kutofaa na yeye atakuwa hafai.

Kwa upande wa miradi ya kilimo cha umwagiliaji, Dkt. Nchemba alieleza kuwa mwaka huu na unaofuata Serikali inaenda kwenye hatua ya kufufua miradi ya umwagiliaji ambapo maeneo mengi ya Wilaya ya Iramba kwa asili yamekuwa yakifaa kwa kilimo hicho.

Alisema, kutakuwa na mitambo kwa ajili ya kuchimba visima na mabwawa ya umwagiliaji na kila kanda itakuwa na mitambo hiyo, hivyo mabwawa yaliyoachwa bila kuendelezwa yatafufuliwa.

Amewataka wananchi  wa eneo hilo kubainisha maeneo yote ambayo yanafaa kwa shughuli hiyo ili mitambo itakapoaanza kufanya kazi iwe rahisi katika utekelezaji.

Vilevile amewataka wananchi wa Kata za Wilaya ya Iramba kutoa ushirikiano kwa viongozi wa chama na Serikali katika kutekeleza majukumu yao ili waweze kutumia muda mwingi kuibua namna bora ya kutekeleza miradi ya maendeleo na kutatua changamoto zao.

Alieleza kuwa Serikali inaendelea na jitihada za kujenga miundombinu ya afya, elimu na maji, hivyo hakuna sababu za kuwa namigogoro ya maeneo ya ujenzi wa miundombinu hiyo kwa kuwa fedha zitakapokuja zitaenda kwenye maeneo ambayo hayana huduma hizo

Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Iramba Magharibi anaendelea na ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika kata za jimbo hilo na kutatua kero mbalimbali za wananchi, miongoni mwa Kata alizotembelewa ni pamoja na Kata ya Ndulungu, Kaselya, Mbelekese na Ndago na miongoni mwa miradi aliyotembelea ni ya maji, shule, barabara na vituo vya afya.

Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Iramba Magharibi Mkoani Singida, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, akihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Ndago, ambapo pamoja na mambo mengine, aliwataka wananchi kubainisha maeneo yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji.
Wazee wa Kijiji cha Ndago wilayani Iramba mkoani Singida, wakimsikiliza kwa makini, Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Iramba Magharibi, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hayupo pichani), alipokuwa akitoa agizo kwa wakaguzi wa ndani kukagua miradi ya maendeleo kwa wakati.
Mzee wa Kijiji cha Ndago, Nzuwamkende Mjungu akimpongeza Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Iramba Magharibi Mkoani Singida, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) kwa jitihada zake zake za kuwaletea maendeleo.
Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Iramba Magharibi Mkoani Singida, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akitoa maelekezo kwa madiwani na viongozi wengine wa Kata za Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, kuhusu usimamizi Madhubuti wa miradi ya maendeleo.

Wananchi wa Kijiji cha Ndago Wilayani Iramba Mkoani Singida wakiwa katika mkutano wa Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Iramba Magharibi Mkoani Singida, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb).

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, (WFM)


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.