Habari za Punde

Alhajj Dk.Hussein Amewataka Wananchi wa Mkwajuni kuitumia na kuitunza vyema misikiti yao kwa kuendelea kutoa sadaka mara kwa mara

 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka wananchi wa Mkwajuni kuitumia na kuitunza vyema misikiti yao kwa kuendelea kutoa sadaka mara kwa mara ili kuwapa nguvu wasimamizi wa misikiti hiyo.

Al hajj  Dk. Mwinyi aliyasema hayo wakati wa ufunguzi wa msikiti wa masjid Istiqama, uliopo Mkwajuni njia ya Matemwe, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema licha ya uzuri wa misikiti na uimara wake lakini itafikia hatua misikiti itahitaji ukarabati, huduma za maji na umeme ambavyo vyote vinahitaji usimamizi mzuri na gharama za kuhudimiwa, hivyo aliwaasa wananchi na waumini wa Kiislamu kutoa sadaka ambazo zitasaidia gharama za uendeshaji pamoja na kuwalipa wasimamizi wa misikiti hiyo

Aidha, aliwaasa waumini hao kuitumia misikiti hiyo kwa sala na ibada nyengine pamoja na kumshukuru mfadhili wa msikiti huo.

Akihutubu kwenye sala ya Ijumaa msikitini hapo, Katibu Mtendaji kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar, Khalid Ali Mfaume alizungumzia fadhila za sadaka kwa muumini mwenye kuitoa na kueleza kuwa sadaka humuweka mtu huru kwa Mola wake.

Aidha, aliongeza sadaka kuleta tahfifu na shifai kwa muumini mgonjwa na kueleza kwamba swadaka huwa sababu ya mja kusamehewa makosa yake kwa Mwenyezi Mungu. Hivyo aliwanasihi waumini hao kushajihika na kuendelea kutoa sana sadaka misikitini mwao.

Mapema, akisoma risala ya ufunguzi wa msikiti huo, Ustadhi Maulid Nafasi Juma alisema ujenzi wa msikiti huo ulitokana na uhitaji wa waumini wa eneo hilo ambao kwa mda mrefu walitumia msikiti mdogo uliokua haukidhi haja ya mahitaji ya eneo hilo.

Ustadhi Nafasi alieleza awali walikua na msikiti uliojengwa tokea mwaka 1983 lakini kutokana na changamoto kadhaa walizokumbana nazo ikiwemo kuongezeka kwa waumini kutokana na kutanuka kwa vijiji kwenye eneo lao, ndio iliwalazimu kutafuta mfadhali kwaajili ya ujenzo mpya hadi kufunguliwa kwake mwaka huu.

IDARA YAMAWASILIANO,

IKULU.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.