Habari za Punde

Uzinduzi wa Kituo cha Mafunzo ya Amali cha Assalaam, Kizimkazi Mkunguni

 Na Maulid Yussuf WMJJWW 

Mkoa wa kusini Unguja.

Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto imesema haitamfumbia macho mtu yeyote anaendelea kuwatelekeza watoto mara baada ya kutengana pamoja na wanaotenda vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia.

Waziri wa Wizara hiyo Mhe Riziki Pembe Juma amesema hayo wakati wa sherehe maalumu ya uzinduzi wa Kituo cha Mafunzo ya Amali cha Assalaam, kiliopo Kizimkazi Mkunguni Mkoa wa Kusini Unguja kilichoanzishwa na bibi Hatice C,olak kutoka nchini Uturuki.

Amesema Serikali ya awamu ya nane chini ya uongozi wa Dkt Hussein Ali Mwinyi itaendelea kupambana na watu hao kama sheria, sera pamoja na miongozo inavyoeleza juu ya matendo hayo.

Amesema Wizara inaendelea kufanya marekebisho ya sheria ya mtoto nambari 6 ya mwaka 2011, ikiwa ni miongoni mwa malengo yake ya  kupambana na watu hao, kwa kuwaweka watoto katika mazingira mazuri na salama.

"Haiwezani eti mtu kazi kuoa na kuacha tu, kila pahala amezaa, halafu kashamuacha mke na watoto pia anao, anawatelekeza bila ya kuwahudumia watoto wale, eti tu kwa kuwa mke ameshamuacha, na sisi Serikali tunasema hatutakuacha, tutakula nawe sahani moja" amesisitiza Mhe.Riziki.

Aidha, Mhe Riziki amewataka wanawake wajane waliomaliza masomo yao ya amali katika kituo hicho, kujiendeleza kwa kujiunganisha vikundi ili kuwe na urahisi katika kuwapatia mikopo au midaada pale inapotokezea kwa lengo la kuwainua kiuchumi.

Amewataka kutambua kuwa Ujane sio sifa wala sio njia ya kuomba omba, bali ni kuw imara katika kujitetea haki zao nkujiendeleza kwa faida yao na watoto wao.

Mhe Waziri ametumia nafasi hiyo kukipongeza Kituo cha Mafunzo ya Amali cha Assalaam kwa kuamua kujitolea kuwafundisha elimu ya amali kina mama wajane na watoto yatima bure ili waweze kujipatia kipato na kuwala vyema watoto wao.

Nae Mkuu wa Kituo cha Mafunzo ya Amali cha  Assalaam ndugu Adnan Issa amesema Kituo hicho kimeanzishwa mwaka 2017 kwa kuwa na jumla ya mama   wajane 42 kutoka Wilaya ya Kusini lakini hadi sasa ni wanafunzi 30 tu ndio wamemaliza na wengine kushindwa kuendelea kutokana na sababu mbalimbali.

Amesema kituo kinatoa kozu za Upishi, uchongaji, ushoni, mafunzo ya Kilimo pamoja na utunzaji wa nyumba (house keeping), lakini kwa mwaka huu wa 2023 wamekusudia kuongeza fani ya ICT, ualimu pamoja na ufundi wa umeme.

Aidha amefahamisha kuwa tayari kwa mwaka huu wanao wanagunzi 50 wakiwemo wajane , mayatima pamoja na baadhi ya vijana waliomaliza kidatu cha nne ambao ni wakaazi wa hpo hapo kizimkazi Mkunguni.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kusini Unguja bwana Rajab Mkasaba amesema Kuanzishwa kwa kituo hicho kunatokana na uongozi thabit wa Rais dkt Hussein katika kuruhusu wawekezaji kuekeza nchini ili kusaidia huduma mbalimbali za kijamii.

Amesema Wilaya yake itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuleta maendeleo nchini.

Ufunguzi wa Kituo cha Amali cha Assalaam cha kizimkazi Mkunguni, umeenda sambamba na zoezi la kuwatunuku vyeti wahitimu 30 waliomaliza mafunzo yao katika fani za upishi, ushoni, uchongaji, kilimo na House keeping.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.