RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka wananchi wa Zanzibar kuzitumia vyema fursa za uwekezaji zilizopo
kwenye maeneo yao ili kujikwamua na changamoto za maisha.
Dk. Mwinyi aliyasema
hayo, Kijini – Matemwe, Mkoa wa Kaskazini Unguja walipofungua hoteli ya nyota
tano ya, Emarald Resort and SPA.
Alisema fursa za
uwekezaji haziwanufaishi wageni pekee, bali wazawa wana nafasi kubwa ya kuzitumia
na jikwamua na ugumu wa maisha ili kuondokana na mkwamo wa maendeleo kwa
kujiongezea kipato na kubadili mfumo wa maisha walionao kupitia fursa hizo.
Alisema wazawa hunufaika
kupitia uzalishaji ikiwemo, uvuvi, kilimo na biashara watakazozizalisha ambazo
zitawalenga wageni waliopo kwenye maeneo yao.
“Kuna faida nyingi tunazozipata
kupitia uwekezaji, zikiwemo ajira, masoko ya bidhaa zetu, na mambo yanayofanywa
na wawekezaji kupitia huduma za jamii jumuishi kama kujenga visima, vituo vya
afya, umeme, barabara ambapo moja kwa moja zinawanufaisha wananchi” Alisema Dk.
Mwinyi.
Alisema Wawekezaji
wameweka imani kubwa Serikalini kwa kuwekeza miradi ya mitaji mikubwa, hivyo
aliwasihi wananchi kuendelea kuwaunga mkono kwa kushirikiana nao katika kuinua
uchumi wa nchi.
Akizungumzia masuala ya
ajira, Dk. Mwinyi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa kipaumbele
cha ajira kwa wazawa wote waliopitiwa na miradi ya uwekezaji na kueleza kuwa asilimia
95 ya ajira zinazotokana na wawekezaji zimelengwa kwa wananchi wazawa kuongeza
kuwa asilimia tano pekee ndio inayobakia kwa mwekezaji hivyo, aliwataka
wananchi kizikimbilia fursa hizo kwa kuonesha uzalendo wakuwapokea wawekezaji kwa
vitendo.
“Niseme kwa wananchi
mara zote tuwe tayari kuwapokea wawekezaji na kuwasaidia ili wao wanufaike na
sisi tunufaike” Aliwasihi, Rais Mwinyi.
Dk. Mwinyi aligusia suala
la kuimarisha miundombinu kijijini hapo ikiwemo maji na barabara, aliwaeleza kwamba
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu ya nane imeweka pesa za kutosha
kuondosha kero za maji na barabara kwa visiwa vya Unguja na Pemba na kueleza kuwa
katika kipindi kitakachojenga barabara nyingi zaidi ni awamu ya nane ambapo
inatarajia kujenga barabara za kilomita 100 hadi 277.
Hata hivyo, aliwaahidi
wanakijiji cha Matemwe kwamba Serikali itawajengea barabara zao za kutoka kibuyuni
hadi kijini na barabara ya round about hadi Nungwi.
Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mudrik Ramadhan
Soraga alieleza kasi ya Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu ya nane imeipa kipaumbele na umuhimu wa pekee sekta
ya Uwekezaji kwa lengo la kuinua uchumi wa nchi na kuendelea kuweka mkazo kwenye
maeneo yote ya uwekezaji.
Kwaupande wake, Mkurugenzi
Mtendaji, Mamlaka ya Uwekezaji na Ukuzaji Vitega Uchumi,
Zanzibar (ZIPA), Sharif Ali Sharif, alisema kwa kipindi cha miaka miwili
kutoka 2021 hadi 2022, Zanzibar imewekeza miradi 223 ikilinganishwa na kipindi
cha miaka sita iliyopita, kutoka 2015 hadi 2020 ambapo miradi 203 iliwekezwa.
Alisema matarajio ya
ZIPA ni kuhakikisha maeneo huru yote ya uchumi, Unguja na Pemba yanakamilika
kwa miundombinu sahihi ili kuendelea kuwakaribisha wawekezaji pamoja na kutoa
huduma mtandao ili kurahisisha ufanisi wa utendaji wao.
Akizungumza kwenye
hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa hoteli ya Emarald Resort and SPA, Bw. Aldo
Scarapicchia alisifu juhudi za Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi kwa ubunifu
wake wakutoa maelfu ya ajira kwa vijana wa Kizanzibari kupita sekta ya utalii
na uwekezaji. Aidha, aliwaahidi Wazanzibari kufanyakazi nao kwa heshima ya
kipekee katika kuendeleza ushirikano uliopo baina yao.
Alisema ukarimu wa
wazanzibari kwa wageni ni heshima kubwa wanayojivunia kwa kipindi chote
walichoingia Zanzibar tokea mwaka 1992 na kuongeza kuwa Zanzibar ni visiwa
vinavyoongoza kwa uzuri kati ya visiwa vya bahari ya Hindi.
IDARA
YA MAWASILIANO -
IKULU,
ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment