Habari za Punde

ALIYEJIFANYA KATIBU WA IKULU MIKONONI MWA POLISI

Ndugu wanahabari, awali ya yote napenda Kumshukuru mwenyezi Mungu kwa kutuamsha salama siku ya leo tukiwa na afya njema na kutuwezesha kufanya shughuri zetu za kujipatia riski kama kawaida.

 Napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dr Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi pamoja na wasaidizi wao waandamizi kwa kuendelea kuongoza vyema nchi yetu. Mpaka sasa Amani na utulivu vimetamalaki  kwani wananchi wanafanya shughuli zao halali za kiuchumi bila ya bughuza wala tishio lolote la kiusalama.

Ndugu Wanahabari, hali ya Usalama kwa Visiwa vya Zanzibar ni shwari hakuna matukio makubwa yenye kuleta taharuki kwa jamii, matukio yanayojitokeza ni ya kawaida na Jeshi la Polisi kwa Kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, tunakabiliana nayo.

Ndungu wanahabari, Jeshi la Polisi Tanzania Kamisheni ya Zanzibar linafanya uchunguzi juu ya matukio mawili ya uhalifu ikiwemo tukio la kughushi nyaraka za Serikali na kuzitumia kuomba visa Ubalozi wa Marekani na tukio la pili ni kujifanya Mtumishi wa Serikali.

Ndungu Wanahabari, Mnamo tarehe 31/01/2023 ofisi ya Kamishna wa Polisi Zanzibar ilipokea taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ofisi ndogo ya Zanzibar, ikieleza kughushiwa kwa nyaraka za Serikali na kuwasilishwa Ubalozi wa Marekani kwa lengo la kuomba visa.

Uchunguzi wa awali uliofanywa na Jeshi la Polisi likishirikiana na vyombo vyengine vya ulinzi pia na Kitengo cha Usalama Ofisi ya Ubalozi wa Marekani nchini imegundua watu 28 waliwasilisha barua wakijitambulisha na kujinasibisha kwamba wao ni watumishi katika Wizara mbali mbali za Serikali ya Mapinduzi Zanzibr. Hivyo kwa barua hizo ambazo zimepitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wameomba kupatiwa Visa kwenda Marekani kufanya shughuli mbalimbali, zikiwemo kuhudhuria semina, masomo n ahata kushiriki michezo.

Ndugu wanahabari, Aidha katika uchunguzi huo watu 12 wamekamatwa na kuhojiwa ambapo baadhi yao wamekiri kutumia mbinu ambazo siyo halali kutaka kwenda Marekani.

Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Ofisi ya Ubalozi wa Marekani Kitengo cha Usalama na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wanaendelea na uchunguzi ubaini mtandao mzima unaohusika na mpango huu wa kusafirisha watu kwenda nje kwa kutumia nyaraka za kughushi.

Napenda nitoe wito kwa vijana na watu wote wanaohitaji kusafiri kwenda nje ya nchi wasitumie njia zisizohalali kufanikisha safari zao na badala yake wafuate taratibu au njia sahihi za kufanikisha safari zao.

Ndungu wanahabari, Jeshi la Polisi vile vile linafanya uchunguzi wa tukio ambalo vijana wawili ambao ni KHATIB KONDO KHATIB miaka 39 mkaazi wa wa Mfenesini Shehia ya Kama Tarishi wa Baraza la Mji Kaskazini B na MDUNGI FADHIL MLEKWA miaka 32, mlinzi katika Wilaya ndogo ya Tummbatu  wamejifanya maafisa wa Serikali

Mnamo tarehe 02/02/2023 Jeshi la Polisi limepokea taarifa kutoka kwa kaimu Mkurugenzi baraza la mji Wilaya ya kaskazini B Mkoa wa Kaskazini UngujaMEMMY KOMBO MCHENGA kwamba alipokea simu kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa yeye ni Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Ikulu akimpa maelekezo ya utekelezaji akimwambia kwamba watumishi aliowaondoa katika nafasi zao awarudishe mara moja ni maagizo kutoka Ikulu.Pia aliongeza kuwa taarifa za Kaimu Mkurugenzi  ziko Ikulu kwamba amemdhibiti sana mkurugenzi kiasi cha kuwa Mkurugenzi hana nafasi na wala hana uwezo wa kutoa maamuzi Zaidi yake yeye.

Ndungu wanahabari, Sambamba na hilo mtu huyo aliyejitambulisha kama ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais alimueleza kaimu mkurugenzi kwamba yeye ana taarifa zake kuwa ni msomi aandae CV zake atakuja kuzichukua ili aangalie jinsi ya kumpatia nafasi kubwa Zaidi kwa sababu Mhe Rais atafanya uteuzi hivi karibuni.

MEMMY KOMBO MCHENGA mara baada ya kupata taarifa hizo aliripoti katika Jeshi la Polisi na uchunguzi ukaanza mara moja. Uchunguzi unaendelea watu wawili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi

Ndugu wanahabari, Wito wangu wananchi tuwe makini na matapeli wa mitandaoni, unapopokea simu au ujumbe wowote kwa mtu ambae humfahamu basi usitekeleze chochote unachoelekezwa na kama kuna mashaka ripoti haraka Jeshi la Polisi. Vijana tusitumie njia za mkato kijipatia kipato, uhalifu haulipi.

Ahsanteni.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.