Habari za Punde

CCM Zanzibar Yawasihi Wananchi Kuendeleza Utamaduni wa Kusoma Vitabu na Machapisho

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa CCM Zanzibar Khadija Ali Salum pamoja na Maafisa wa idara hiyo  wakiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani katika Maktaba Kuu ya Zanzibar iliyopo Maisara Unguja.
MKURUGENZI wa bodi ya huduma za maktaba Zanzibar Dkt. Ulfat Abdul-Aziz Ibrahim, akieleza namna wanavyotoa huduma ya usomaji wa vitabu mbalimbali katika taasisi hiyo.
MKURUGENZI wa bodi ya huduma za maktaba Zanzibar Dkt. Ulfat Abdul-Aziz Ibrahim, akieleza namna wanavyotoa huduma ya usomaji wa vitabu mbalimbali katika taasisi hiyo.

MKURUGENZI wa bodi ya huduma za maktaba Zanzibar Dkt. Ulfat Abdul-Aziz Ibrahim(kulia), akizungumza juu ya muundo wa utendaji wa Maktaba hiyo baada ya Katibu wa Mkuu wa Idara ya SUKI Khadija Ali Salum (upande wa kushoto) kufika ofisini kwake kwa ajili ya ziara maalum ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025.

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa CCM Zanzibar(SUKI) Khadija Ali Salum,amewasihi wananchi kuendeleza utamaduni wa kutembelea maktaba mbalimbali nchini ili kujifunza na kusoma vitabu ,machapisho,nyaraka na taarifa zitakazowaongezea maarifa na uelewa yakinifu.

Wito huo ameutoa katika ziara yake ya kutembelea Maktaba Kuu ya Zanzibar iliyopo mtaa wa Maisara Unguja.

Alisema wananchi wanatakiwa kuwa na utamaduni wa kusoma vitabu na machapisho mbalimbali ili wawe na uelewa juu ya mambo tofauti yanayohusu Zanzibar, Tanzania bara,Afrika na duniani kwa ujumla.

Katika maelezo yake Katibu huyo wa SUKI Khadija,alieleza kuwa Maktaba Kuu ya Zanzibar imehifadhi nyaraka,machapisho na vitabu mbalimbali vinavyosaidia kuwajengea uwezo wa kitaaluma wanafunzi wa ngazi mbalimbali za kitaaluma na kwamba wananchi nao wanatakiwa kuchangamkia fursa hiyo.

Kupitia ziara hiyo Khadija, aliahidi kuwa Chama Cha Mapinduzi kitatafuta ufumbuzi wa baadhi ya changamoto za kiutendaji zinazoikabili taasisi hiyo ambayo ni chimbuko la kuhifadhi nyaraka muhimu za kitaaluma.

Alieleza kuwa licha ya kuwepo na changamoto za kiutendaji wafanyakazi wa taasisi hiyo wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii ili waende sambamba na kasi ya utendaji wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi.

Pamoja na hayo alisema lengo la ziara hiyo ni kufuatia maazimio ya kikao cha kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025 kilichofanyika februari 20,mwaka 2023 hapo Afisi kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar.

Alisema kuwa pamoja na majukumu yanayoikabili taasisi hiyo wanatakiwa kuongeza juhudi katika kutekeleza kwa ufanisi majukumu ya maktaba kuu yaliyoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

“Maana halisi ya maktaba ni sehemu ya jengo lenye nyaraka au machapisho ya kujifunza na kujisomea hivyo kwa maana hiyo kila mwananchi ana wajibu wa kujiongezea maarifa kupitia maktaba hiyo.”alisema Khadija.

Naye Mkurugenzi wa Maktaba Kuu Zanzibar Mkurugenzi wa huduma za Maktaba Zanzibar Dkt. Ulfat Abdul-aziz Ibrahim, amesema wanatoa huduma mbalimbali za kuwasaidia wanafunzi na wananchi kwa ujumla kupata vitabu ili wajifunze na kupata taaluma,elimu na maarifa juu ya mambo mbalimbali yaliyowazunguka.

Alisema kupitia taasisi hiyo inayofanya kazi zake Unguja na Pemba wanahifadhi vitabu mbalimbali vikiwemo vya maalum za uchumi,sayanzi,maarifa ya jamii,diplomasia na ujasiriamali na mambo mengine yanayohusu viumbe hai na visivyo hai.

Alizitaja changamoto zinazowakabili katika maktaba hiyo kuwa ni pamoja na udogo wa jengo la maktaba hiyo pamoja na ukosefu wa vifaa vya huduma za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA).

Dkt.Ulfat, alizitaja changamoto nyingine kuwa ni upungufu wa huduma ya mtandao ‘Internet’, upungufu wa wakutubi na ukosefu wa usafiri kwa watendaji wa taasisi hiyo hasa wakati wanapokuwa na majukumu ya nje ya ofisi hiyo.

Kupitia ziara hiyo Mkurugenzi huyo alisema kwa sasa taasisi hiyo inatakiwa kwenda sambamba na mabadiliko ya sayansi na teknolojia kwa kuhakikisha huduma za maktaba zinatolewa katika mfumo wa kisasa.

“Tunatoa huduma bora na rafiki kwa wateja wetu na wananchi kwa ujumla hivyo wananchi,wageni na wanafunzi wa ngazi tofauti milango yetu ipo wazi tunawakaribisha waje kujiongezea maarifa,elimu,taaluma na uelewa”. Alisema Mkurugenzi huyo.

Mkurugenzi huyo alifafanua kuwa baada ya Waziri wa Elimu Tanzania bara kupiga marufuku baadhi ya vitabu visivyozingatia maadili na kwa upande wa Zanzibar katika maktaba hiyo walifanya uchunguzi na kubaini uwepo wa baadhi ya vitabu hivyo na kuhakikisha wanaviondoka katika mfumo na taratibu za huduma ya usomaji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.