Serikali ya Tanzania inaendelea kutekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa kushirikiana na nchi mbalimbali duniani ili kukuza uchumi wa nchi kupitia fursa za biashara, uwekezaji na utalii zilizopo ndani na nje ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, Bungeni leo tarehe 09 Februari,2023 wakati akijibu swali la Mhe. Felista Njau, Mbunge wa Viti Maalum kuhusu umuhimu wa Serikali wa kuainisha nchi zenye fursa za biashara na uwekezaji ili kukuza pato la Taifa.
Amesema Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kushirikiana na Wizara za kisekta na Balozi za Tanzania imeendelea kutangaza fursa za biashara na uwekezaji zenye manufaa kwa Taifa na kwamba Wizara inaandaa Mpango wa Kitaifa wa kutekeleza Diplomasia ya Uchumi utakaojumuisha Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ili kufikia malengo tarajiwa.
Amesema Mpango huu ambao unatarajiwa kukamilika kabla ya mwezi Desemba 2023, pamoja na mambo mengine unalenga kuhakikisha fursa za biashara, uwekezaji na utalii zinakuwa na tija zaidi kwa wananchi wa Tanzania. Pia Mpango huo utajumuisha Sekta zote husika ikiwa ni pamoja na kuainisha maeneo muhimu ya kisekta yatakayo changia katika kukuza uchumi na pato la Taifa.
Akichangia hoja kuhusu mkakati wa utoaji elimu kwa wananchi kuhusu dhana ya Diplomasia ya Uchumi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax, amesema Wizara inaendelea kutoa elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali na kufafanua kwamba Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi unaoandaliwa pia utajumuisha Mpango wa kutoa elimu kwa umma kuhusu dhana hiyo ili kuwawezesha wananchi kuielewa dhana hii na kuwawezesha kutumia fursa mbalimbali zinazotokana na ushirikiano kati ya Tanzania na nchi mbalimbali.
Kuhusu taarifa hasi zinazotolewa na vyombo vya kimataifa dhidi ya Tanzania, Mhe. Dkt. Tax amesema tayari Wizara imeanza kushirikiana na vyombo vya habari vya Nje hususan vile vinavyorusha matangazo yake kwa Kiswahili ili kupitia vyombo hivyo fursa na taarifa chanya kuhusu Tanzania zitangazwe duniani kote.
No comments:
Post a Comment