Habari za Punde

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar yatoa elimu ya kisheria Matemwe

Wakili wa Serikali mwandamizi kutoka Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar Hamisa Mmanga, Akiwasisitiza wanajamii wa kijiji cha Matemwe Kaskazini Unguja kuzisajili kisheria ardhi wanazozimiliki kama njia muhimu ya kupunguza migogoro ya adhi nchini.
Wakili wa Serikali kutoka afisi ya Mwanasheria Mkuu Mbarouk Suleiman Othman akiwasilisha mada kuhusu Majukumu ya Afisi ya Mwanasheria Mkuu katika ziara ya kutoa elimu ya Sheria kwa wananchi wa kijiji cha Matemwe, Mko wa Kaskazini Unguja.
 Mmoja wa wanakijiji Makame Mati akichangia katika mada zilizotolewa na Mawakili wa Serikali huko katika kijiji cha Matemwe, ikiwa ni shamra shamra ya wiki ya Sheria Zanzibar. Picha na Faki Mjaka


Na Faki Mjaka, Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar

Wakili wa Serikali mwandamizi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar Hamisa Mmanga, amewashauri wanajamii kuhakikisha ardhi wanazozimiliki zinasajiliwa kisheria kama njia muhimu ya kupunguza migogoro ya adhi nchini.

Amesema migogoro ya ardhi kwa sasa imepamba moto kutokana na kuongezeka kwa thamani ya ardhi, hivyo inaposajiliwa kisheria ni vigumu mtu mwingine kujiingiza na kudai ardhi hiyo ni yake.

Wakili Hamisa alitoa ushauri huo katika Kijiji cha Matwemwe Mkoa wa Kusini Unguja wakati akiwasilisha mada katika ziara za kutoa elimu ya kisheria kwa jamii (outreach program) ikiwa ni mwendelezo wa shamra shamra za Wiki ya Sheria Zanzibar ambayo huadhimishwa mwezi wa Februari ya kila mwaka.

Ziara hiyo iliyoandaliwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ilikuwa na lengo la kuwafahamisha wananchi sheria mbalimbali ili wazifamu. Kuzifahamu sheria hizo kutasaidia kupunguza migogoro ikiwemo ya Ardhi, vitendo vya udhalilishaji, madawa ya kulevya na uhalifu katika jamii.

Akiifafanua kwa undani Sheria ya umiliki wa Ardhi Namba 12 ya mwaka 1992 Wakili hamisa alisema Sheria hiyo inamtaka Mtu anayemiliki ardhi aisajili.

“Kwa hiyo nasisiza kusajili Ardhi ni lazima, lakini tukiishi kuwa wazee wetu waliishi bila kusajili Ardhi yao na sisi tuishi hivyo itapelekea migogoro ya kila siku. Hata kama una ardhi ya kurithi nenda kaisajili kisheria, kabla hawajatokea watu wakadai ni yao”Alisisitiza Wakili Hamisa.

Aidha aliwataka wananchi hao kutowaruhusu wale wote wanaovamia Maeneo yao katika hatua za awali, badala ya kuwaacha kuanza kujenga ndio waanze harakati za kuwaondoa katika maeneo yao.

“Wakati mwingine migogoro tunaitanua wenyewe, unamuona Mtu ameanza kuvamia eneo lenu, hamumuondoshi mapema. Munamuacha anaendelea tu hadi kuanza hatua za kujenga ndio hapo munaaza kumkataza, ni ngumu. Mvamizi wa ardhi vyema kupambana naye katika hatua za awali kabisa” Alisema Wakili Hamisa.

Wakili Hamisa amewapongeza wananchi wa Matemwe kwa kuitikia wito na kujitokeza kwa wingi kusikiliza elimu iliyotolewa kutoka Afisi hiyo.

Kwa upande wake Wakili wa Serikali kutoka afisi ya Mwanasheria Mkuu Mbarouk Suleiman Othman wakati akiwasilisha mada kuhusu Majukumu ya Afisi ya Mwanasheria Mkuu aliwafahamisha pia wananchi kuhusu haki yao ya kuweza kuishitaki Taasisi yoyote ikiwemo ya Serikali pale wanapodhani haki zao zimechukuliwa na taasisi hizo.

Kupitia sheria ya mwenendo wa mashtaka ya madai (government proceeding act,kifungu Namba sita, kifungu kidogo cha tatu) kinaelezea utaratibu mzima wa kuishitaki Taasisi ya serikali ambapo Mwananchi kabla ya kuishitaki Serikali analazimika kutoa Notisi ya siku 60 kuhusu azma yake hiyo katika Ofisi ya Mwanansheria Mkuu.

Wakili Mbarouk alieleza kuwa malengo ya kuwekwa Notisi ya siku hizo 60 ni kuipa serikali muda wa kujitathmini ili kama kuna mgogoro wowote uweze kutatuliwa ndani ya siku hizo kabla ya kupelekana Mahakamani moja kwa moja.

Hivyo Wakili Mbarouk ametoa wito kwa wananchi hao kuitumia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kupeleka malalamiko yao ya Msingi pale ambao wanadhani kuna taasisi imewanyima haki zao.

Kwa upande wake Wakili kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka DPP Issa Ahmed wakati akiwasilisha Mada ya madawa ya kulevya na athari zake aliwataka wananchi hao kuendelea kuwafichua watu wanaofanya biashara hiyo kutokana na madhara yake mengi katika jamii.

“Nataka nikuhakikishieni kuwa tutamulinda, hatutotoa siri, kama kuna mtu anafanya biashara ya madawa tufahamisheni au lifahamisheni Jeshi la Polisi na hatua zitachukuliwa” Alisema Wakili Issa.

Katika mada nyingi zilizowasilishwa na Wanansheria hao, wananchi wengi wa Matemwe waliguswa zaidi na mada ya Migogoro ya ardhi ambayo wamedai ndio inayowasumbua kijijini kwao.

Makame Wadi kutoka kijiji cha Matemwe alizishukuru taasisi za Mwanasheria Mkuu na DPP kwa elimu waliyowapatia na kusisitiza kuwa elimu hiyo inatakiwa itolewe mara kwa mara hasa ya migogoro ya ardhi ili watu wapate haki zao na kuishi kwa Amani.

“Kwa kweli tunakushukuruni sana kwa elimu lakini muda hutoshi, huku tunaumia zaidi na migogoro ya ardhi, watu wanajimilikisha maeneo yasiyokuwa yao. Mnatakiwa muje mara kwa mara mutusikilize na kutufahamisha badala ya kuja mara moja kwa mwaka”.

Wiki ya Sheria mwaka huu imeanza Febuari 6 na kilele chake kinatarajiwa kuwa Febuari 13, ambapo Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar katika kuadhimisha siku hiyo wamefanya ziara za kutoa elimu ili kuisaidia jamii kuwa na ufahamu wa maswala ya kisheria jambo litakalosaidia kupunguza migogoro na uhalifu nchini.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.