RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi amepiga
marufuku kwa wafanyabiashara kusafirsha bidhaa za vyakula vyote vinavyoingia
nchini kutolewa nje ya nchi.
Alhajj Mwinyi alitoa marufuku hiyo wakati akiwatubia wananchi na waumini wa
Kiislam walipotekeleza ibada ya sala ya Ijumaa huko Masjid Shifaa -
Mwembetanga, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha, aliwaagiza wafanyabiashara kutoa chakula chote kilichomo kwenye
maghala badala ya kukifungia ili kuepusha uhaba wa chakula nchini na kukwepa
kuongeza bei.
Alhajj Mwinyi, alisema kitendo walichokifanya wafanyabiashara hao cha kufungia
chakula kwenye maghala kimeleta athari kubwa kwa wananchi wa visiwa vya Unguja
na Pemba na kueleza kwamba Pemba kulikua na hali mbaya zaidi ya upungufu wa
chakula hata hivyo, alieleza baada ya kufanya mazungumzo na wafanyabiashara
mbalimbali wa bidhaa na vyakula hali ya sasa kwa Pemba imetengemaa.
“Nimewaambia wafanyabiashara Serikali si vyema ikafanya biashara lakini
mkitufikisha sehemu lazima tufanye biashara nitawaambia Serikali na Shirika la
biashara la ZSTC watoe fedha walete wao chakula wauze, kwasababu hatuwezi kuwavumilia
wafanyabiashara kuongeza bei kwa makusudi kwa kupenda wao huku wanaumiza watu”
Alionya Al hajj Mwinyi.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuchukua hatua
mbalimbali kuhakikisha chakula zinaendelea kushuka bei nchini.
Akizungumzia kuelekea mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, Al hajj Mwinyi
alitoa agizo kwa wafanyabiashara hao kuongeza chakula cha kutosha ili kuepuka
uhaba wa chakula hasa kwenye bidhaa muhimu za unga, mchele, sukari na mafuta ya
kupikia na kueleza kuwa hadi sasa bandarini kuna meli zenye tani hadi 10 za
chakula zikiendelea kushusha mizigo.
Rais Dk. Mwinyi alieleza, licha ya changanoto ya wafanyabiashara
waliochangia kupanda kwa bei za vyakula ambapo alieleza tabia za baadhi ya
wafanyabiashara kupandisha bei au kuhodhi mali kuonekane kuna uhaba wa bidhaa
ili wapandishe bei pia alieleza tatizo jengine ni ufanisi mdogo wa bandari, meli
kukaa sana bandarini kabla ya kushusha mizigo.
Al hajj Mwinyi aliongeza Serikali inampango madhubuti wa kuhakikisha
bandari inaongezewa ufanisi wa hali ya juu ili kutoa fursa kwa mizigo hasa ya
chakula kushushwa haraka ili vyakula viendelee kuwepo sokoni.
Akizungumzia masuala ya kuimarisha afya na kufanya mazoezi, Alhajj Mwinyi,
alieleza Kutofanya mazoezi kunachangia
magonjwa yasioambukiza yakiwemo presha, moyo na saratani hali aliyoieleza
kurudisha nyuma maendeleo ya taifa.
“Imethibitika kwa utafiti kwamba moja ya sababu inayochangia magonjwa
yasioambukiza ni kutofanya mazoezi, tujitahidi kufanya mazoezi ili tulinde afya
zetu” Alishauri Al hajj Mwinyi.
Aliwataka wananchi kujenga tabia ya kufanya
mazoezi kila siku pamoja na kuwaasa kupunguza kula vyakula vinavyochochea zaidi
magonjwa hayo.
Alisema taifa lenye watu wasiokuwa na afya haliwezi kupata maendeleo, sababu
hospitali zitajaa wagonjwa na uwezo wa serikali utapungua kwa kutibu watu
badala ya watu hao kuzalisha kuiongezea kipato Serikali.
Alisema wananchi wamejijenga utamaduni wa kupanda
gari kila sehemu wanazokwenda hali aliyoieleza kutotoa fursa kwao ya kufanya
mazoezi nakuongeza kuwa kutembea sana kwa gari badala ya miguu kunachochea magonjwa hayo kwa kiasi kikubwa.
Akihutubu kwenye sala ya Ijumaa msikitini hapo, Katibu Mtendaji kutoka
Ofisi ya Mufti Zanzibar, Khalid Ali Mfaume aliwataka waumini wa dini ya kiislam
kuchukua tahadhari na kuwa makini na shari za hamasa za kushajihisha ushoga
duniani.
Alisema dunia imeharibika na kuenea kwa mawakala wanaoshajihisha uchafu huo
kila kona hivyo, alieza hatua iliyofikia sasa kila kitu kinachoshabihiana na
mfumo wa maisha ya mwanadaamu kuwekewa
nembo ama alama ya kushajihisha ushoga na kutolea mfano kwenye mavazi yakawaida
kama nguo, mikanda, viatu na kwenye mahitaji ya lazima ya binaadamu.
Aidha, aliwaasa wazazi na walezi majumbani kuwa makini kufuatilia mienendo
ya watoto wao, ikiwemo michezo na vitu vya kuchezea wanavyowanunulia pamoja na
kuwaeleza kuwa makini na katuni wanazopenda kuangalia watoto ili kuhakikisha
mazingira ya watoto hao hayaathiriwi na mfumo na hamasa za kishetani
wanaohubiri ushoga.
Hata hivyo, aliongeza kusema mabadiliko ya uchumi na kupanda kwa gharama za
maisha hazijasababishwa na uchumi pekee bali, dhambi za walimwengu na vitendo
vichafu vya ushoga na udhalilishaji kijinsia vimechangia kukwamisha ugumu wa
maisha duniani.
Msikiti wa Masjid Shifaa - Mwembetanga,
ulizinduliwa raism na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al
hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi tarehe 07/05/2021 .
IDARA YAMAWASILIANO,
IKULU
No comments:
Post a Comment