Habari za Punde

Mweleko wa mvua za masika: Jamii ielimishwe njia bora za kukabiliana na maafa

 Na Khadija Khamis -Maelezo 10/03/2023.

 

Wenyekiti na Makatibu wa kamati za maafa wa wilaya za Unguja wametakiwa kuandaa mipango mikakati ya kuelimisha jamii njia bora za kukabiliana na maafa hasa kipindi hichi cha muelekeo wa mvua za masika ili kuepusha athari zitazojitokeza.

 

Akifungua kikao cha siku moja cha kujadili mwelekeo wa mvua za masika katika ukumbi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa, Maruhubi Naibu katibu Mkuu Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Salhina Mwita Ameir amesema hatua hiyo itasaidia wananchi kujua njia bora za kujiepusha na athari kwa kujikinga na kuchukua hatua stahiki pindi majanga yanapotokea katika maeneo yao.

 

Amesema kumekuwa na athari nyingi zinazojitokeza katika msimu wa mvua za masika ambazo huathiri watu na mali zao kutokana na mafuriko,yanayosababisha kuharibu makaazi ya watu, miundombinu ya barabara,umeme, maji,mripuko wa maradhi ajali za barabarani, upepo mkali,radi na kadhalika.

 

Aidha alieleza kuwa pindi mvua kubwa za masika zikitokea nidhahiri kwamba kuna maafa yatajitokeza ambayo hayawezi kuepukika lakini kuna uwezo wa kupunguza athari iwapo elimu ikitolewa mapema kwa jamii.

 

Akitoa taarifa ya Utabiri wa hali ya hewa Mwakilishi kutoka Mamlaka ya hali ya hewa (TMA) Hassan Khatib Ame amesema mfumo wa hali ya hewa  unaonyesha hivi sasa joto la bahari katika eneo la kitropiki ya bahari ya pasifiki liko chini ya wastani.

 

Aidha alisema muelekeo wa mvua za masika kwa mwezi Machi hadi Mei kwa visiwa vya Unguja na Pemba vitakuwa na mvua ya wastani hadi juu ya wastani na kuna uwezekano wa mvua hizi kufikia  hadi mwezi wa Juni .

 

Nae  Mkuu wa Divisheni ya Mawasiliano na Tahadhari za Mapema Omar Ali Mohamed amesema mvua za masika zinazotarajia kunyesha zinaonekana zitakuwa ni kubwa hivyo ni vyema wananchi kuwa na tahadhari ili kupunguza athari za majanga yanayoweza kujitokeza.

 

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Makame Khatib Makame amewataka wananchi hasa wale wanaishi katika maeneo hatarishi kuchukua hatua mbadala ili kujinusuru na maafa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.