Akizungumza kwenye ghafla ya uzinduzi wa
Bohari ya mafuta Mangapwani, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amezitaka Wizara
zinazohusika kuziambia kampuni zote za mafuta kuelekeza shughuli zote za mafuta
kwenye eneo hilo.
"Serikali imekusudia kampuni
zote za mafuta kushushia mafuta yao hapa Mangapwani" Alisema D.k Mwinyi.
Alisema hatua za awali za ujenzi wa bandari
hiyo ni kuanza kwa ujenzi wa barabara kubwa ya kilomita 60 ambayo alieleza
itakuwa barabara ya kwanza kubwa na yenye ubora kwa Zanzibar na uwezo wa
kuhudumia magari makubwa ya kubebea mizigo mizito kulingana na uhalisia wa
bandari yenyewe.
Dk. Mwinyi alisema bandari jumushi ya
Mangapwani itahusisha bandari ya makontena itakayokuwa na gati ya urefu wa
kilomita moja itakayohudumia sio Zanzibar pekee bali ukanda mzima wa Afrika
Mashariki na makontena yatakayoshushwa bandarini hapo yaende hadi Dar es
Salaam, Mombasa, Beira hadi Durban Afrika Kusini yakitokea Zanzibar.
"Tunataka bandari hii
isihudumie Zanzibar pekee, tunataka Dar es Salaam, Mombasa, Beira hadi Durban Afika Kusini waitumie bandari hii " alieleza
Dk. Mwinyi.
Bandari nyengine inayotarajiwa kujengwa eneo
hilo Dk. Mwinyi alieleza ni bandari ya nafaka itakayohusisha ushushwaji wa
bidhaa zote za vyakula ikiwemo mchele, maharage, mahindi, unga wa ngano na
vyakula vyengine ambavyo vitashushwa kwa muda mchache ili viwafikie wananchi
kwa wakati, ujenzi mwengine ni wa bandari ya mafuta itakayohifadhi lita milioni
21.
Rais Dk. Mwinyi alieleza bandari nyingine
itakayojengwa kwenye eneo hilo ni bandari ya uvuvi itakayokidhi Sera ya Uchumi wa
Buluu nchini, alisema bado Serikali haijavuna vyakutosha rasilimali za bahari
na ujenzi wa bandari ya kisasa ya uvuvi inalengo la kuleta meli kubwa
zitakazovuna vizuri matunda ya baharini wakiwemo Samaki wakubwa.
Vilevile Dk. Mwinyi alieleza Serikali inatarajia
kuwa na mafuta ya kutosha na kuweka akiba ili Zanzibar iuze mafuta hadi nchi
nyingine zisizokuwa na bahari na ujenzi wa bandari jumushi ya Mangapwani ni
ufumbuzi wa changamoto zizilizopo kwenye bandari ya Malindi ambako meli hutumia
siku 5, 7 hadi 10 kushusha mizigo hiyo, hali inayosababisha kupunguza uchumi wa
nchi.
Akizungumzia kwenye hafla hiyo Waziri wa Maji,
Nishati na Madini, Shaib Hassan Kaduara alisema Wizara hiyo inagusa maisha ya
watu ya kila siku na kueleza nia ya Serikali kuwaondoshea wananchi
changamoto zote zinazotokana na masuala ya maji, umeme na mafuta.
Alisema katika jitihada za Serikali kupunguza
kero hizo, inatarajia kuzindua tangi kubwa la maji safi na salama Chakechake
Pemba, lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni moja ambalo litakua la kwanza
kwa ukuwa kwa Zanzibar nzima.
Naye, Mkurugenzi wa masuala ya ushirika wa
makampuni ya Bakhresa, Hussein Sufiani aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kwa kuweka mazingira mazuri ya kufanya biashara na kutatua changamoto
zinazowakabili wafanyabiasha pamoja na kuwafanikishia mradi wao huo wa Bohari
ya Mafuta ya Mangapwani.
Aliihakikishia Serikali kwamba kampuni za
Bakhresa zitaendelea kushirikiana na taasisi za Serikali zinazohusika na
usimamizi wa majukumu yao ya kila siku na kuahidi kuendelea kutoa huduma bora
kwa wateja wao.
Baadae Rais Dk. Mwinyi alifanya ziara ya
kushtukiza kwa kutembelea ujenzi wa mtaro Meli Kumi njia ya Bumbwini, ujenzi wa
Soko la Chuini na Soko la Jumbi na Mwanakwerekwe kukagua ujenzi na maendeleo ya
miradi hiyo ilivyofikia. Pia alitembelea eneo la waanika madagaa, Mangapwani.
IDARA YA MAWASILIANO
IKULU, ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment