Habari za Punde

Wizara ya Kilimo Zanzibar yaridhishwa Utekelezaji wa AGRI-CONNECT kuwainua Wakulima.


Maafisa kutoka Wizara ya Kilimo na wataalam kutoka kwenye miradi inayotekelezwa chini ya mpango wa AGRICONNECT wakikagua changamoto zinazolikabili zao za Vanilla kwenye shamba la mkulima Juma Abrahman Khatib kupitia mradi wa VIUNGO Zanzibar lililopo Shehia ya Piki, Wilaya ya Wete Kaskazini Pemba.
Maafisa wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar pamoja na wataalamu kutoka kwenye miradi inayotekelezwa kupitia program ya AGRICONNECT kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (eu) wakipokea maelezo kutoka kwa mkulima wa Nyanya wakati wa ziara. 
Dkt. Suleiman Shehe, afisa mkuu wa Utafiti wa wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar akipokea maelezo kutoka kwa ALI KHAMIS ABDALLA,  mkulima wa mboganna matunda Shehia ya Kwale, Wete

WIZARA ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo Zanzibar imepongeza hatua zinazochukuliwa na wadau wa maendeleo katika kukuza na kuimarisha thamani ya kilimo cha Viungo, Mboga na Matunda Zanzibar kupitia miradi inayotekelezwa nchini.


Hayo yamebainika kufuatia ziara ya kutembelea wakulima wanufaika wa miradi inayotekelezwa na programu ya AGRI-CONNECT Tanzania kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) iliyofanyika Kisiwani Pemba kwa lengo la kutathimini hali ya utekelezaji wa programu hiyo katika kukuza uzalishaji wa mazao hayo kwa wakulima.


Katika ziara hiyo iliyoongozwa na Dkt. Suleiman Shehe, afisa mkuu wa Utafiti wa wizara hiyo, alisema juhudi kubwa zinazochukuliwa na watekelezaji wa miradi hiyo inasaidia kuongeza thamani ya mazao hayo ambayo kwa muda mrefu yamekuwa hayapewi kipaumbele kama sehemu ya shughuli muhimu za kiuchumi kwa wananchi na taifa.


Alifahamisha kuwa wananchi wengi walikuwa bado hawaoni umuhimu wa kujiingiza katika kilimo cha mazao ya mboga na matunda kama chanzo muhimu cha kujiongeza kiuchumi lakini kupitia taaluma ambayo miradi hiyo imeitoa imewaamsha wakulima wengi kuanzisha mashamba yao.


Aidha aliwata watekelezaji wa miradi hiyo kuwekeza nguvu zaidi katika kuwezesha wakulima kukabiliana na changamoto zinazowakabili hasa miundombinu ili waweze kufikia malengo ya uzalishaji kwa wingi bila kiwazo.


“Niwapongeze tumefanya kazi kubwa ya kutoa elimu ya kilimo na kupitia ziara hii wote tumejionea kwamba wakulima sasa elimu ya kilimo tayari wanayo ya kutosha. Nitoe rai yangu, sasa tuelekeze nguvu zetu kuwawezesha wakulima hawa kupata miundombinu bora ili waweze kutumia elimu hii tuliyowapatia kuzalisha kwa wingi na hatimaye kujikwamua kimaisha kupitia kilimo hiki,” alisema Dkt. Shehe.


Aidha alihimiza pia miradi kuweka mkazo kwa wakulima kuzingatia suala la uwekaji kumbukumbu ya shughuli zao ili kuwawezesha kujua gharama za uendeshaji na faida zake kwenye shughuli hizo.


Kwa upande wake Omar Mohamed, ambaye ni afisa mshauri wa miradi ya AGRI-CONNECT Zanzibar alisema kuna haja ya miradi kujua mbinu gani za kutumia kuwashawishi vijana kujiingiza katika kilimo ili kuachana na dhana potofu ya kuona kilimo kama mateso kwao.


Alisema, “wakati tunaendelea kutekeleza miradi hii, tutazame zaidi shughuli ambazo zinawagusa vijana moja kwa moja ili iwe rahisi kwao kuvutika na kuja katika uzalishaji wa shughuli za kilimo na lengo letu waondokane na dhana mbaya ya kuona kilimo hakiwezi kuwasaidia kukuza uchumi wao.”


Ali Abdalla, afisa tathimini na ufuatiliaji wa mradi wa VIUNGO, alisema licha ya juhudi kubwa zinazochukuliwa na miradi kukuza kilimo Zanzibar, lakini bado nguvu ya serikali kushirikiana na wadau wengine inahitajika ili kufanya tafiti ya changamoto zinazokwaza wakulima ikiwemo udongo na maradhi nyemelezi kwenye mazao.


"Bado kuna ‘gap’ (utofauti) kubwa sana kati ya watekelezaji wa mradi ya kilimo na wizara kuhusu masuala ya utafiti wa maradhi ya kilimo jambo ambalo linapelekea hasara kwa wakulima.”

 

Miongoni mwa wakulima waliotembelewa ni pamoja na Hassan Shamte, ambaye ni mkulima wa Migomba katika Shehia ya Mgagadu Wilaya ya Mkoani, mnufaika wa mradi wa VIUNGO na kushudia namna mradi huo unasaidia kuendeleza kilimo cha Matunda kupitia njia za kisasa.


Mkulima huyo alieleza kupitia mradi huo alipatiwa elimu ya uzalishaji bora wa matunda, taaluma ambayo imemsaidia kuanzisha shamba lake mwenyewe la migomba na Parachichi lenye ukubwa wa zaidi ya ekari moja.


Kuhusu uendelevu wa shughuli baada ya mradi kumaliza muda wake alisema, "elimu na mbegu za Miparachichi na migomba tuliyopata kwenye mradi huu ni urithi wa kudumu kwetu. Tunashukuru taaluma tuliyoipata imetufanya tuamini katika kile tunachokifanya na hata siku mradi ukiwa haupo tutaendeleza kile tulichofunzwa."


Katika ziara hiyo, jumla ya maeneo 18 ya wanufaika wa miradi inayotekelezwa chini ya program ya AGRI-CONNECT kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) ikiwa ni pamoja na mradi wa VIUNGO unaotekelezwa na People’s Development Forum (PDF), Community Forests Pemba na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TANZANIA , Zanzibar (TAMWA ZNZ) yalitembelewa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.