Habari za Punde

Uharibifu wa mazingira ni changamoto kubwa ya nchi na dunia

 


Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amesema kwamba uharibifu wa mazingira  ni changamoto kubwa ya nchi na dunia kwa jumla, lakini athari zake kubwa zinabebwa nchi masikini ikiwemo Zanzibar.

Mhe. Othman ameyasema hayo kwa nyakati tofauti huko Wete na Micheweni Mkoa Kaskazini Pemba, alipozungunza na watendaji na wafanyakazi wa Halmashauri ya Micheweni na wa Baraza la Mji wa wete na Masheha katika ziara yake ya kuelezea mpango wa serikali wa kuirejesha  na kurithisha Zanzibar kuwa ya kijani.

Amesema kwamba hivi sasa maji ya bahari yamekuwa yakiingia katika arthi kavu na kuathiri shughuli za kilimo na nyenginezo za kibinaadamu kwa sababu kina ya bahari kimekuwa kikipanda kwa kasi sehemu mbali mbali duniani kutokana na changamoto kubwa ya uharibu wa mazingira na ongezeko la joto.

Aidha Mhe. Othman amesema kwamba nchi za Visiwa kama Zanzibar  na maeneo yaliyozungukwa na bahari ndio waathirika wakubwa wa tatizo hilo kutokana na kuyeyuka kwa theluji  duniani baada ya kupanda kima cha joto sehemu mbali mbali za duani.

Mhe. Makamu amesema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa makusudi imeamua kuja na mpango wa kukabiliana na hali ya uharibifu wa mazingira na kuirejesha Zanzibar kuwa ya kijani ambao ni mkakati shirikishi wa Serikali na wananchi,  viongozi na taasisi mbali mbali ili kujenga utamaduni mpya wa kuwarithisha vijana kupenda kupanda miti na kuihifadhi.

Amesema kwamba serikali inaelekeza juhudi kubwa katika  mpango huo kwa wananchi kwa vile wao ndio wenye dhamana ya kutengeneza mwelekeo mpya utakaosaidia kuendeleza juhudi za utamaduni kwa wananchi wa kupanda miti pamoja na kuwarithisha vijana utamaduni huo ili kulinusuru taifa na janga la kimazingira.

Aidha amesema kwamba hatua hiyo pia inakusudia kuwajengea utamaduni wananchi kuacha kukata miti ovyo kwa matumizi ya shughuli mbali mbali ikiwemo za kilimo ili kuepusha nchi kuwa na ukame na kukumbwa na tatizo la ukosefu wa huduma ya maji.

Amesema kwamba hivi sasa kina cha maji kimepungua sana katika maeneo mbali mbali kama vile za mabonde ya Zanzibar yaliyokuwa na kiasi kikubwa cha maji ya kutosheleza mahitaji   kutokana na kuwepo kasi kubwa ya mabadiliko ya tabia nchi na binaadamu.

Amesema kwamba maeneo mengi yaliyokuwa na mito mikubwa na maji ya kutosha hivi sasa yamekauka kabisa jambo ambalo limechangia kuepo uhaba wa maji kwa kuwa hata hayo yanayopatikana yanalazimika kutafutwa katika visima vya kina kirefu.

Ameongeza kwamba  ni lazima wananchi kuwa na utamaduni mpya wa kuacha kuyageuza majangwa maeneo ya mapori kwa kuikata miti ovyo na badala yake waendeleze juhudi za kupanda miti kwa kuanza hatua za kupanda miti kwenye nyumba zakuishi.

Aidha amewakumbusha wananchi kwamba miti ni uchumi mkubwa iwapo juhudi zitafanyika kwa kuwa miti mingi inayopandwa katika kipindi kifupi inaweza kuuzwa kwa thamani kubwa kutokana na mahitaji yanavyongezeka siku hadi siku.

Naye Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Ndugu Matar Zahor Masoud, amesema kwamba ni vyema wananchi wakajiweka tayari katika kutekeleza mpango huo utakapoanza kwa kuwa ni jambo muhimu litakaloinusuru nchi isiharibike zaidi kimazingira.

Amefahamisha kwamba katika kufanikisha mpango huo ni busara jamii ikatanabahi kwa kuwaanda watoto katika utamaduni mpya wa kuanzisha utaratibu wa kupanda na kuhifadhi miti tangu wakiwa skuli katika hatua za awali hadi wanapomalizia ili wazoee na kukua na utamaduni huo.

 

Mwisho.

Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kupitia Kitengo chake cha habari leo tarehe 07.03.2023.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.