Na Fauzia Mussa. Maelezo Zanzibar
Wakala wa chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) wamelifungia ghala iliyokua ikihifadhi bidhaa mbalimbali ukiwemo mchele kutokana na ghala hiyo kukosa sifa za kuhifadhia bidhaa za vyakula.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa kushtukiza kuangalia usalama wa chakula,na uhalali wa uwepo wa ghala hilo huko Mpendae Kaimu Mkurugenzi Idara ya usalama wa chakula ZFDA Bi.Khadija Ali Sheha amesema ukaguzi huo umebaini kuwa ghala hilo halijasajiliwa na haliko katika hali ya usafi na haliruhusu hewa kupita hali inayopelekea chakula kinachihifadhiwa hapo kutokua salama.
Alisema kuwa usalama wa chakula ni jukumu la kila mmoja hivyo ameitaka jamii kutoa taarifa mapema mara tu wanapoona hali isiyokuwa ya kawaida katika maghala ya kuhifadhia chakula
"Kwa pamoja sasa tushirikiane kulinda Afya zetu kwa kuyafichuwa maghala kama haya ambayo yanahatarisha Afya za watu na kuitia hasara Serikali" alishauri kaimu huyo.
Aidha katika ukaguzi huo ZFDA wamebaini kuwa mmiliki wa ghala hilo amekua akiziba vifungashio vya asili kwa baadhi ya bidhaa zilizozuiliwa kusafirishwa nje ya Zanzibar ikiwemo mchele aina ya mapembe katika maboksi na vipolo ili kurahisisha usafirishaji Jambo ambalo ni kosa kisheria.
Kwa upande wake mmiliki wa ghala hilo Bw.Saleh Hassan Khamis amesema kuwa amekua akizifunga tena bidhaa hizo katika mapolo na maboksi ili kuzihifadhi na kuziweka salama wanapokua safarini bila kufahamu kufanya hivyo kama ni kosa kisheria, hivyo Bw.Saleh ameiomba ZFDA kuwapatia elimu Wafanyabiashara ili kuepuka makosa yasiyotarajiwa.
Nae Sheha wa Shehia ya Mpendae Bw.Suleiman Ali Makuu amewasihi wafanya Biashara kuwa waaminifu na kuwataka wafuate Sheria zilizowekwa na Serikali ili kuepuka matatizo wakati wanapofanya Biashara zao.
Katika Ukaguzi huo mbali na bidhaa nyengine jumla ya polo mia tatu za mchele aina ya mapembe yenye ujazo wa kilo hamsini yamekutikana katika ghala hilo ambalo halijasajiliwa.
No comments:
Post a Comment