RAIS wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi
amejumuika kwenye futari ya pamoja na wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja
ikiwa ni kawaida yake kufuturu na wananchi kila mwaka katika kutekeleza ibada
ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Katika hafla
hiyo iliyofanyika ukumbi wa Chuo cha Mafunzo ya Amali, Mkokotoni wilaya ya
Kaskazini A, Unguja alikowaandalia futari wananchi wa Mkoa huo imehudhuriwa pia
na Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi, Mama Mariam Mwinyi.
Al hajj Dk.
Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi wa Mkoa wa Kaskazini kwa
mwitikio mkubwa waliomuonesha kujumuika nae kwenye futari ya pamoja
aliyowaandalia.
“Leo ni siku
yetu ya kwanza tangu tumeanza kufutarisha, tumeanza na Mkoa huu wa Kaskazini
Unguja, nawashukuru wananchi nyote kwa muitikio muliouonesha, ushirikiano wenu
tokea maandalizi hadi kukamilika kwa shuhuli yetu….”
“….Unapowaalika
watu na wakakuitikia basi hunabudi kutoa shukurani kwao, nawashukuru sana nyote
kwa ushiriki wenu na kwa niaba ya wenzenu hakika mumewawakilisha vyema wenzenu,
nayaona makundi yote mupo hapa” Alieleza Al hajj Dk. Mwinyi.
Akizungumza
kwenye halfa hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala
Bora, Haroun Ali Suleiman alisifu jitihada za rais Dk. Mwinyi katika
kuungamkono masuala ya dini na kushajihisha mambo yenye heri na maendeleo ya nchi.
Alisema
taifa linamshughudia anavyoshiriana na wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba
kwenye mambo mbalimbali ya kijamii na hairati, ikiwemo kushiriki kwenye ibada
za sala za jamaa maeneo tofauti ya visiwa vya Zanzibar, kufungua misikiti
pamoja na kufutari pamoja na wananchi wake jambo alilolieleza ni la kupigiwa
mfano kwa kiongozi wan chi na kumsifu Dk. Mwinyi kwamba ni Rais wa watu wote.
Kwa upande
wao, wananchi wa mkoa huo wamesifu juhudi za maendeleo zinazofanywa na awamu ya
nane ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kueleza kasi ya maendeleo ya mkoa
huo imezidi maradufu.
Walisema
maendeleo kwenye sekta ya miundombinu ikiwemo maji safi, barabara na kiwanja
cha ndege ndani ya mkoa huo zimefungua fursa nyingi za uchumi na maendeleo katika
usatawi wa mkoa wao.
Akizungumza
kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mkuu wa Mkoa huo, Ayoub Mohamed
Mahmoud alisema Mkoa huo unazidi kufunguka kimaendeleo kwa kuimarika na
kuongezeka kwa huduma za maji safi, afya, elimu, kilimo, ujenzi mkubwa wa
bandari jumuishi ya Mangapwani, huduma hizo zina badari ya Mkokotoni.
Alisema, kukua
kwa sekta ya utalii kwenye mkoa huo na biashara ndogondogo zimeufungua mkoa
kibiashara na uwekezaji.
“Tunakushukuru
na kukupongeza kwa dhati kwa kutuandalia futari hii wananchi wa Mkoa wa Kaskazini
pia tunakupongeza kwa kazi kubwa ya maendeleo unayoifanya kwenye Mkoa wetu” Alishukuru
RC Ayoub.
IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment