Habari za Punde

Dkt Jafo: Ni Muungano wenye mafanikio lukuki

 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar unaotimiza miaka 59 leo umekuwa na mafanikio lukuki.

Amesema hayo leo Aprili 26, 2023 ambapo ametaja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kuimarika kwa uchumi, huduma za kijamii zikiwemo afya, elimu, maji na uanzishwaji wa Ofisi za Taasisi za Muungano Zanzibar.

Dkt. Jafo ametaja mafanikio mengine kuwa ni kuimarika kwa ulinzi na usalama, utekelezaji wa programu na miradi ya maendeleo kwa pande zote mbili za Muungano, utatuzi wa changamoto za Muungano, kuimarika kwa ushirikiano kwa masuala yasiyo ya Muungano na utoaji wa elimu ya Muungano kwa umma.

Amesema mafanikio hayo yameendelea kuwanufaisha wananchi wa pande mbili za Muungano na hivyo kuwezesha Muungano wetu kuendelea kudumu kwa zaidi ya nusu karne.

“Tuna kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuulinda Muungano wetu kwani ni Muungano wa kipekee uliodumu kati ya majaribio kadhaa ya aina hiyo barani Afrika hivyo, nitoe rai kwa Watanzania wenzangu wote tuendelee kuuenzi, kuulinda na kuudumisha Muungano wetu, kwa kuwa ndiyo siri ya mafanikio yetu,” amesisitiza.

Ameongeza kuwa Muungano huu ni wa damu zaidi kwani wananchi wa pande zote mbili wanachanganyika na kufanya shughuli za kijamii pamoja bila kubaguana hivyo uemeendelea kudumu hadi leo.

Aidha, Waziri Jafo amewaasa Watanzania kuendelea kujali mazingira kwa kupanda miti na kufanya usafi ili kuuenzi na kuudumisha Muungano huu adhimu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.