Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Amekabidhi Tuzo Maalum ya Kuendeleza Sekta ya Maji Afrika

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushirika wa Maji Duniani Kanda ya Afrika Kusini Rais Mstaafu wa Tanzania Mhe.Dk. Jakaya Mrisho Kikwete akimkabidhi TUZO Maalum ya Watu Mashuhuri Waliota Mabadiliko Chanya katika Sekta ya Maji Afrika Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi  hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 5-4-2023
 

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema itaendeleza juhudi  kuhakikisha maeneo yote ya Zanzibar yanafanikiwa na kufikiwa na maji safi na salama kwa usatawi wa jamii na uchumi wa nchi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi aliyasema hayo Ikulu Zanzibar kwenye hafla fupi ya kukabidhiwa tunzo maalum ya watu mashuhuri walioleta mabadiliko chanya katika kuendeleza sekta ya maji Afrika, iliyotolewa na taasisi ya kimataifa ya Global Water Changemakers kwenye Kongamano la Umoja wa Mataifa nchini Marekani Machi 22 mwaka huu ambayo alikabidhiwa na Rais Mstaafu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, awamu ya nne Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.

Dk. Mwinyi alisema jitihada kubwa zinazochukuliwa na Serikali kuleta mageuzi kwenye sekta ya maji, Zanzibar zitasaidia kustawisha jamii kwa kupatikana huduma za uhakika na endelevu za maji safi na salama.

“Ahadi yangu ni kuwa Serikali itaendeleza juhudi zake za kuhakikisha maeneo yote ya Unguja na Pemba yanafanikiwa na yanafikiwa kuwa na huduma ya maji safi na salama kwa usatawi wa jamii.” Aliahidi Rais Dk. Mwinyi.

Alisema uhaba wa maji nchini unachangia umasikini unaowasababishia watu kutumia muda mwingi kutafuta maji badala ya kufanya shughuli nyengine za maendeleo, hivyo aliahidi serikali itafanya kila linalowezekana kuhakikisha inayafikia matarajio ya wananchi ya kupata huduma ya maji safi na ya uhakika.

Rais Dk. Mwinyi alieleza hatua tatu mihimu zitakazoondosha changamoto sugu  ya maji Zanzibar endapo zitatekelezwa kwa wakati na watendaji wa sekta hiyo ikiwemo kupanga mipango mizuri na kuitekeleza kwa wakati.

Pia rasilimali watu wenye uwezo, weledi na ufanisi kutengeneza miradi, kuisimamia na kuitekeleza hadi kuikamilisha kwa msada wa rasilimali fedha ambayo itasaidia kufanikisha mipango waliyojiwekea.

“Zanzibar ni ndogo tukisema tunalivalia njuga jambo hili kuondoa tatizo la maji Unguja na Pemba inawzekana sana na tutanza kwa fedha za serikali na baadae kuwaomba wadau wetu kutusaidia ili kukamilisha nchi nzima,” alibainisha.

Alisema mpango wa Zanzibar wa uwekezaji wa maji uliandaliwa kwa kuzingatia matakwa ya ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2020/2025, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050, kupitia ahadi alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi Mkuu pamoja na mipango ya maendeleo iliyopangwa katika jumuiya za kikanda na kimataifa.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi aliipongeza tasisi ya Global Water Partnership kanda ya Afika Kusini kwa kuwaunga mkono kufanikisha mpango wa uwekezaji wa sekta ya Zanzibar (2022 -2023) ambao umeipatia heshima kubwa hadi kutunukiwa tunzo hiyo kwa niaba ya serikali na wananchi wa Zanzibar, nakuongeza kuwa ni hatua ya kuunga mkono jitihada za serikali katika kuleta mabadiliko na mageuzi kwenye sekta ya maji Zanzibar.

Naye Rais Mstaafu Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushirika wa Maji duniani kanda ya Afrika ya Kusini, alimpongeza Rais Mwinyi kwa kupokea tunzo hiyo aliyoieleza ni ishara ya jumuiya za kimataifa kutambua jitihada zinazofanywa na Rais na serikali yake kuimarisha sekta ya maji Unguja na Pemba, pia alieleza tunzo hiyo imeipa heshima Zanzibar kimataifa na kuifanya Zanzibar kuwa ni kichocheo cha kuendeleza maji barani Afrika.

Mpema, Waziri wa Maji, Nishati na Madini, Shaibu Hassan Kaduara, alieleza tunzo ya Rais Mwinyi ni juhudi alizozifanya ndani ya miaka miwili ya uongozi wake ambapo Serikali imefanikiwa kuzalisha maji lita milioni 149 wakati awali zilizalishwa lita milioni 46 tu za maji. Pia kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake Serikali imefanukiwa kulaza miundombinu yam aji kilomita 3,129 wakati awali ilikua kilomita 2001 tu ya miundombinu hiyo.

Tunzo hiyo maalum ya watu mashuhuri walioleta mabadiliko makubwa kwenye sekta ya maji barani Afrika, yenye lengo la kutambua michangoi ya viongozi wa Afrika, kuthamini jitihada mbalimbali wanazofanya kwenye masuala ya maji,  ilianzishwa na benki ya dunua, inafanya kazi zake na Shirika la kimataifa la Global water Partership la Sweden ambalo linalifanyia kazi zake kwa Kanda tano za Afrika, ikiwemo kanda ya Afrika Mashariki, Afrika Kaskazini, Afrika Kusini, Afrika ya Kati na Afrika ya Magharibi na Dk. Jakaya Kikwete amepewa dhama ya kuratibu masuala ya maji kwa Kanda ya Afrika Kusini.

Machi 22 mwaka huu, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi na Rais Mstaafu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete na viongozi wengine wa nchi za Senegal, Namibia, Uholanzi na Zambia walipewa tunzo hizo kwa kutambua mchango wao wa kusimamamia na kuleta mabadiliko chanya katika kuendeleza sekta ya maji duniani.

IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.