RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameishukuru Serikali
ya China kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa Tanzania ikiwemo Zanzibar kwenye
masuala mbalimbali ya maendeleo.
Dk. Mwinyi ametoa
shukurani hizo Ikulu, Zanzibar alishuhudia utiaji wa shaini mikataba ya
miradi mitano ya ushikirikano kwenye sekta ya afya baina ya Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China.
Katika hafla hiyo Rais
Dk. Mwinyi alisema, Zanzibar imenufaika na fursa nyingi za maendeleo kupitia
misaada tofauti inayoletwa kutoka China hasa sekta za Afya na Elimu ikiwemo
Tanzania kujifunza uzoefu wa masuala mbalimbali ya afya, kupokea timu za
madaktari bingwa wanaofika nchini kwaajili ya kubadilishana uzoefu na wazawa
hali aliyoieleza imeimarisha uhusiano mwema uliopo baina yao.
Alisema mikataba
minne aliyoishuhudia sio tuu itaimarisha huduma za tiba nchini pekee, lakini
itajenga ushirikiano mwema baina ya maofisa wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar na China jambo alilolieleza ni ishara ya uhusiano mwema uliopo baina
ya mataifa mawili hayo.
Rais Dk. Mwinyi
alieleza, uhusiano wa China na Tanzania utakumbukwa zaidi kwa kuinufaisha
Zanzibar kupitia sekta ya afya katika suala zima la kuimarisha miundombinu ya
afya, vifaa tiba, dawa mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa wataalamu wa afya
wazawa, pamoja na timu za madaktari bingwa wanaofika Zanzibar kila mwaka kwa
nyakati tofauti na Tanzania kwa ujumla, jambo alilolieleza kwamba limeimarisha
uhusiano wa China na Tanzania.
Aidha, Dk. Mwinyi
alimpongeza Balozi mdogo wa China aliepo Zanzibar, Zhang Zhisheng kwa kazi
kubwa anayoifanya ya kukuza ushiriiano uliopo baina ya China na Zanzibar.
“Wenzetu China mmetusaidia sana hata tukieleza
hatutomaliza, nimeshuhudia utiaji wa saini mikataba minne ya ushirikiano baina
ya Zanzibar na China, kupitia sekta ya afya, miradi hii itaendelea kuimarisha ushirikiano
wetu uliopo” Alisifu Dk. Mwinyi.
Naye,
Rais wa taasisi ya Ushirikiano baina ya Afrika na China, (CAPFA) Dk. Li Bin ameeleza
miradi hiyo itatatua maradhi sugu jamii hasa kina Mama na kutoa fursa za miradi
mbalimbali itakayonufaisha pande zote za ushirikiano wa Nchi hizo na
kuboresha huduma za sekta ya Afya.
Dk. Li pia aliisifu Tanzania kwa ukaribu wa kihistoria baina yake na China alioueleza ni wa mda mrefu tokea uhai wa Mwenyekiti Mao Zedong na Mwl. Julius Kambarage Nyerere, zaidi ya miaka 50 iliyopita.
Alisema, Tanzania
imebarikiwa kuwa na raia wenye ukarimu, upendo na ushirikiano, ambao ni
kielelezo chema kwenye kukuza uhusiano uliopo baina yao na China.
Alieleza, ushirikiano
huo ni mwendelezo wa fikra njema za waasisi wa mataifa mawili hayo, Mwenyekiti Mao
Zedong na Mwl. Julius Kambarage Nyerere na kueleza Serikali ya Jamhuri ya watu
wa China inajivunia uhusiano huo kwa maendeleo makubwa yaliyofikiwa na watu wa
China na Tanzania ikiwemo kukuza uhusiano wa jamii na uchumi.
Akizungumza kwenye
hafla hiyo, Waziri wa Afya, Nassor Mazrui alisema mikataba waliyoisaini mbele
ya Rais Dk. Mwinyi itagharimu dola za Marekani 4,76,000 sawa na Shilingi
bilioni 1.2 za Tanzania.
Miongo mwa miradi
iliyosainiwa ni pamoja na mradi wa Ushirikiano wa hospitali baina ya China na
Afrika, Utafiti na udhibiti wa magonjwa ya kitropiki ikiwemo Kichocho,
Uchunguzi wa saratani ya shingo ya mlango wa kizazi na kituo cha matibabu ya
Mama na Mtoto pamoja na msaada wa vifaa tiba.
Aidha, hospitali zitakazonufaika
na ushirikiano huo ni hospotali kuu, Mnazi Mmoja, Kivunge, Chake chake na
Abdallah Mzee Pemba.
IDARA YA MAWASILIANO,
IKULU - ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment