RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiagana na mgeni wake Balozi wa Canada Nchini Tanzania.Mhe.Klye Nunas, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar .
SERIKALI ya Mapinduzi
ya Zanzibar imesema ina nia ya dhati ya kujinufaisha zaidi na matunda ya
baharini kupitia sera yake ya Uchumi wa buluu kwa kuvuna mengi zaidi kuliko
inavyoendelea kunufaika ili kuimarisha uchumi wa nchi.
Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo Ikulu,
Zanzibar alipozungumza na Balozi wa Canada nchini Tanzania, Kyle Nunas aliefika
kumtembelea.
Alisema, kupitia
sekta ya uchumi wa buluu Zanzibar pia inanufaika na biashara kupitia bahari kwa
mipaka jirani ya Dar es Salaam, Tanga, Mombasa na na visiwa jirani vikiwemo
Comoro.
Aidha, Rais Dk.
Mwinyi alimueleza balozi huyo kwamba Utalii ni sekta namba moja ya uchumi wa Zanzibar
ambapo alisema Serikali imejikita kuimarisha miundombinu yote ikiwemo ujenzi wa
babdari jumuishi ya Mangapwani ambayo itatoa fursa zaidi za uchumi, kutanua uwanja
wa ndege wa kimataifa wa Abeid Amani Karume kwa kuongeza jengo jipya la
(Terminal 4), kuboresha barabara, kuongeza hoteli za kisasa na nyumba za wageni
pamoja na kuimarisha vivutio vya utalii.
Dk. Mwinyi alieleza, Zanzibar
kwasasa inapokea ndege nyingi za kimataifa kiasi cha kuongeza idadi kubwa ya
watalii nchini, pia alimueleza mgeni wake huyo kwamba Serikali ina nia ya
kulifufua eneo kongwe la hoteli ya bwawani kwa kujengwa kumbi kubwa za mikutano
kwaajili ya watalii ili kuongeza mapato ya nchi.
Akizungumzia sekta za
afya na elimu, Rais Dk. Mwinyi alimueleza balozi huyo kwamba Serikali pia
inaendelea kuboresha upatikanaji wa huduma bora hasa kwenye maeneo ya vijijini
ili kujenga uwiano sawa wa huduma na sehemu za mijini.
Kwa upande wa afya,
Rais Dk. Mwinyi alieleza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inazingatia
kukuza huduma ya afya ya kinga kwa mama na mtoto na mapambano dhidi ya magonjwa
ya kuambukiza.
Alisema, uhisusiano
wa diplomasia baina ya Tanzania na Canada ni wa muda mrefu pia alieleza
Zanzibar ikiwa sehemu ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, imefaidika na
uhusiano huo hasa kupitia sekta za Afya na Elimu.
Akizungumza kwenye
hafla hiyo, Balozi Kyle Nunas ameisifu Tanzania ikiwemo Zanzibar kwa kubarikiwa
kuwa na amani na utulivu na siasa za kistaarabu katika kuimarisha ustawi wa nchi
yake.
Balozi Kyle Nunas
alimueleza Rais Dk. Mwinyi, kwamba Canada inaungamkono zaidi masuala ya haki za
binaadamu hasa kwa makundi maalumu wakiwemo wanawake wa wasichana ambapo
imeelekeza sera na miradi mingi kwenye eneo hilo.
Alisema Canada
imevutiwa zaidi na ustaarabu wa Tanzania hasa katika kuimarisha demokrasia,
uhuru wa vyombo vya Habari pia balozi huyo alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba
nchi yao inavutiwa kuiona Tanzania inavyoendeleza siasa za kistaarabu na
mazungumzo ya busara kwa kambi pinzani.
IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment