Habari za Punde

SMZ Inajivunia Ushirikiano Mzuri Ulipo Baina Yake na India

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na mgeni wake Balozi Mdogo wa India anayefanyia kazi Zanzibar Dr.Kumar Praveen ,aliyefika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar .
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akiagana na mgeni wake Balozi Mdogo wa India anayefanyia kazi Zanzibar Dr.Kumar Praveen ,aliyefika Ikulu Jijini Zanzibar leo baada ya mazungumzo yao.
 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema sekta ya Maji safi na salama ni muhumu katika ustawi wa jamii na maendeleo ya ukuaji wa uchimi Zainzibar.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo Ikulu Zanzibar, alipozungumza na Balozi mdogo wa India aliepo Zanzibar, Dk. Kumar Praveen, aliefika kujitambulisha.

Rais Dk. Mwinyi alisema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar bado inajivunia ushirikiano mzuri ulipo baia yake na India na kwamba Zanzibar imekua ikinufaika na fursa mbalimbali kutoka India ikiwemo fursa za masomo ya muda mrefu na mfupi pamoja miradi ya maji.

Pia Dk. Mwinyi ameishukuru Serikali ya India kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa kwa SMZ hususan, ufadhili wa Miradi ya maji inayotekelezwa kupitia mkopo wa Benki ya Exim ya India.

Akizungumzia ujenzi wa Chuo Kikuu cha Teknolojia cha IIT, kinachotarajiwa kujengwa Zanzibar kwa Ushirikiano wa Serikali ya India, Rais Dk. Mwinyi alimueleza Balozi Praveen kwamba mazungumzo baina ya SMZ na wahadhir kutoka taasisi ya Teknolojia ya “India Institute of Technology (IIT) yanaendelea vizuri na wapo kwenye hatua nzuri ya mpango huo kwaajili ya utekelezaji wake.

Alisema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeridhishwa na kasi ya uanzishwaji wa taasisi hiyo kwa Zanzibar ambayo inatarajiwa kuanza mwezi Oktoba mwaka huu kwa ushiriano wa pande mbili hizo na wadau wengine wa Serikali na kueleza kuwa wanaunga mkono hatua hiyo itakayoleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya elimu, Zanzibar yatakayonufaisha pia ukanda wa Afrika Mashariki na Afrika kwa jumla. 

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Kumar Praveen, Balozi mdogo aliepo Zanzibar aligusia Miradi ya Maji Zanzibar inayofadhiliwa na Serikali ya India, mradi wa Chuo cha Ufundi wa Amali, Pemba pamoja na ufadhili wa masomo kwa watumishi wa Zanzibar nchini India.

Vile vile, Balozi Praveen alimweleza Rais Dk. Mwinyi kuhusu ujio wa Waziri wa Mambo ya nje ya India, Dk. Subrahmanyam Jaishankar anayetarajiwa kuwasili nchini mwezi Julai mwaka huu, kwa ajili ya uzinduzi wa Miradi ya Maji Zanzibar, katika ujio wake huo Dk. Subrahmanyam pia anatarajiwa kufika Dar es Salaam na Dodoma.

Uhusiano wa diplomasia uliopo baina ya Tanzania na India ni wa historia ambapo India ilifungua Ubalozi wake Dar es Salaam mwezi Novemba mwaka 1962 na mwaka 1974 ikafungua ubalozi mdogo Zanzibar.

Ushirikiano baina India na Tanzania umeendelea kuimarika kwa fursa nyingi za maendeleo kupatikana kwa watu wa mataifa mawili hayo.

Tanzania inaongoza kwa kupata msaada wa nafasi nyingi za udhamini wa masomo nchini India kuliko nchi nyenyine yoyote barani Afrika kutokana na ushirikiano mzuri uliopo baina ya mataifa mawili hayo.

IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.