Habari za Punde

Waziri Pembe Amempongeza Mwakilishi Mkaazi wa UNICEF Kwa Ushirikiano Wake

Na Maulid Yussuf WMJJWW 

Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Zanzibar Mhe Riziki Pembe Juma amekutana na kuagana na Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto Duniani UNICEF  bibi Sharlin Bahuguna 

Hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Rais Kazi Uchumi na Uwekezaji Mwanakwerekwe mjini Unguja ambayo imehudhuriwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe Anna Athanas Paul pamoja na Katibu Mkuu bi Abeida Rashid Abdallah na baadhi ya  wakurugenzi wa Wizara hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Waziri amemshukuru Mwakilishi huyo kwa kufanya nae kazi kwa mashirikiano ya pamoja katika kuhakikisha wanaendeleza miradi yao mbalimbali waliyoianziasha kwa lengo la kuwalinda watoto na wanawake nchini.

Aidha amesema suala la udhalilishaji wa watoto bado ni  changamoto, hivyo amemuahidi kuendelea kusimamia na kuwalinda watoto juu ya masuala hayo, kwani  ndio misingi bora ya Taifa la baadae.

Naye Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto Duniani UNICEF bibi Sharlin Bahuguna ameipongeza Wizara kwa ushirikiano mzuri waliompa katika kipindi chote chautekelezaji wa majukumu yake.

Pia ameshukuru kwa kukamilisha mipango ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiwemo mpango wa Kitaifa wa kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto Zanzibar 2017-2022.  

Pia amesema kuwa mpango mwengine ni  utekelezaji wa programu za uimarishaji wa malezi hasa Familia bora, Taifa imara pamoja na  Programu ya Premero  na kuahidi kuendeleza ahadi za kikazi chenye usawa kupitia malezi na makuzi ya awali ya mtoto ECD. 

Hata hivyo bibi Sharlin ameahidi kuendeleza ushirikiano wake  wakati akiwa nje ya  Tanzania kwa kuhakikisha kuwa shughuli zinazopangwa na Serikali zinatekelezwa kikamilifu.

Pia amemuhahikishia Mhe Waziri  kuwa Wataendelea kubadilishana uzoefu kadri watakavyohitajika.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto bi Abeida Rashid Abdallah amesema Wizara inahitaji kupanga mipango madhubuti ili kuona adhma ya  programu mbalimbali ikiwemo ya  Uimarishaji wa malezi hasa Familia bora Taifa imara, yanafikiwa.


Bibi Sharlin Bahuguna amemaliza muda wake wa miaka 5 akiwa ni  Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto Duniani UNICEF.
Mwisho. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.