RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali
Mwinyi amesema sekta za Afya, Maji na Elimu ni muhimu kwa ustawi wa watu wa
Zanzibar.
Dk. Mwinyi aliyasema
hayo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na Kaimu Balozi wa Saudi Arabia nchini,
Fahad Alharbi aliefika kumtembelea.
Rais Dk. Mwinyi alisema,
licha ya sekta hizo kuwepo kwa kiwango kikubwa nchini lakini zinahitaji
kuimarishwa zaidi ili kuwaondoshea wananchi changamoto zinazozikabili sekta
hizo, hivyo aliiomba Serikali ya Saudi Arabia kuongeza ushirikiano zaidi kwenye
sekta hizo.
Aidha, Dk. Mwinyi
aliishukuru Serikali ya Saudi kwa zawadi ya tende, tani 25 iliyoletwa kwa ajili
ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kueleza Serikali inaweka utaratibu
mzuri ili iwafikie walengwa.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi
ameeleza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekua na ushirikiano wa karibu wa
maendeleo na taasisi mbalimbali za kimataifa za umma na binafsi, hivyo
alizikaribisha taasisi nyengine kutoka Saudi Arabia kuisaidia Zanzibar.
Naye, Kaimu Balozi wa
Saudi Arabia, Fahad Alharbi akiambatana na ujumbe wa watu wanne kutoka Taasisi
ya misaada ya kibinaadamu ya King Salman wa Saudi Arabia, aliahidi kuendelea
kuudumisha ushirikiano wa Diplomasia uliopo baina ya Zanzibar na Saudi Arabia
ambao ni wa historia.
Alieleza, Serikali ya
nchi hiyo imekua ikitoa misaada kwa sekta mbalimbali kwa mataifa mengi duniani.
Pia Kaimu Balozi huyo,
alitumia fursa hiyo kumfikisha Rais Dk. Mwinyi salamu za Mfalme wa Saudi
Arabia, Salman bin Abdulazizi Al Saud na kueleza kuwa salamu za Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar pia atazifikisha kwa Mfalme huyo.
Mapema, ujumbe kutoka
Taasisi ya misaada ya kibinaadamu ya King Salman wa Saudi Arabia, ulikutana na
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Mhe.
Haroun Ali Suleiman ofisini kwake Mazizini na kumkabidhi katuni 1,200 za tende
sawa na tani 25 kwa ajili ya zawadi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment