Habari za Punde

Waziri Balozi Dkt.Chana Azindua Mfumo wa Kidigitali wa Usajili wa Vyama vya Michezo

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana  (katikati) akibonyeza kitufe kuashiria Uzinduzi wa Mfumo wa Kidigitali wa Usajili wa Vyama vya Michezo , Julai 20, 2023 jijini Dar es Salaam.
Wanaoshuhudia ni  Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Saidi Yakubu, Kaimu Mkurugenzi wa Michezo, Ally Mayay Tembele, Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Bi. Neema Msitha na Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza hilo, Bw. Leodgar Tenga.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana  (katikati), akipokea mwongozo wa Usajili Kidigitali  wa Vyama vya Michezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza la Michezo Tanzania  (BMT) Bw. Leodgar Tenga, mara baada ya kuzindua Mfumo huo  Julai 20 2023 Jijini Dar es Salaam.
Wanaoshuhudia ni  Katibu Mkuu wa Wizara  Bw. Saidi Yakubu, Kaimu  Mkurugenzi wa Michezo Ally Mayay Tembele, Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Bi. Neema Msitha na Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza hilo Bw. Leodgar Tenga.

Na Shamimu Nyaki

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana leo Julai 20, 2023 jijini Dar es Salaam amezindua Mfumo wa Kidijitali wa Usajili wa Vyama na Mashirikisho ya Michezo.

Akizungumza kabla ya kuzindua Mfumo huo, Mhe. Chana amelipongeza Baraza la Michezo la Taifa kwa hatua hiyo ambayo imewarahisishia wadau hao utekekezaji ambapo pia amepongeza kwa kutoa mafunzo kwa wadau hao namna bora ya kuendesha michezo.

"Nitoe wito kwa wadau wa michezo kurasimisha shughuli zao kwa kusajili Taasisi, Akademi, Vituo, Vilabu, Vikundi, Vyama na Mashirikisho kwa kuwa sasa usajili unafanyika kwa urahisi", amesisitiza Mhe. Chana

Awali akimkaribisha Waziri, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Saidi Yakubu amesema hivi sasa Tanzania inashiriki michezo mingi Kimataifa ambapo katika michezo ya All Africa Games itashiriki riadha, ngumi, judo na soka la wanawake huku akieleza kuwa, hivi sasa sekta ambazo zitakuwa zinajishighulisha katika uwekezaji na utekekezaji wa miradi ikiwemo ya nishati na madini katika kurudisha kwa jamii pia itachangia katika kuendeleza michezo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza hilo, Bw. Leodgar Tenga amesema uzinduzi huo umeambata na mafunzo ambayo yalikuwa na mada mbili, moja ni Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi katika michezo na Utaalamishaji wa Michezo ambazo zilipata wachangiaji mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.