SERIKLI ya Mapinduzi ya
Zanzibar, imesema itaendelea kutenga bajeti ya mikopo kuwasaidia
vijana wanaokosa fursa ya kujiunga na elimu ya juu ili wafanikishe ndoto zao
kwa ustawi wa maendeleo yao.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameyasema hayo kwenye maadhimisho ya siku ya
vijana kimataifa, viwanja vya Maisara Suleiman Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini
Magharibi.
Alisema, Serikali imejipanga kufanikisha lengo lake hilo licha ya ongezeko la kila mwaka la
vijana wanaopata sifa za kujiunga na elimu ya juu.
Alisema, Serikali imechukua jitihada mbali mbali kuimarisha ustawi wa
vijana kwa kuwashirikisha kwenye sekta zote za Maendeleo ikiwemo Afya, Elimu,
Kilimo, Uvuvi, TEHAMA, Ujasiriamali na michezo kwa kuwawesha kujiajiri na
kuajiriwa.
Aidha, Dk. Mwinyi alieleza Serikali za SMZ na SMT zimeweka utaratibu maalum wa ajira, chini ya
Sheria ya Utumishi wa Umma nambari 2/2008 ambayo imetoa asilimia 21% ya Ajira
kwa Vijana wa Zanzibar kwenye Sekta za Muungano.
Alisema, kwa mujibu wa taarifa ya muelekeo wa
Kiuchumi ya mwaka 2022 kupitia miradi ya fedha za ahueni za UVIKO 19, jumla ya vijana
13,870 walifanikiwa kupata ajira za muda kupitia miradi iliyowekezwa na Serikali
kupitia sekta mbalimbali za maendeleo.
Alieleza, mbali na jitihada za kuanzisha Wizara na Idara Maalum ya kushughulikia
Maendeleo ya Vijana ili kuimarisha usimamizi na uratibu wa shughuli za
Maendeleo yao nchini pia Serikali imeanzisha Sera ya Maendeleo ya Vijana ya
Mwaka 2005 iliyoweka miongozo ya shughuli zote za Maendeleo na Ustawi wao.
Akiizungumzia maendeleo ya sekta ya Afya kwa vijana,
Rais Dk. Mwinyi alisema Serikali
kupitia Wizara ya Afya imekua ikishirikiana na wadau wa maendeleo wakiwemo shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu ulimwengu
(UNFPA) kwa pamoja wameanzisha na kuviendeleza vituo 13 vya huduma rafiki za
Afya kwa Vijana kwa wilaya zote za Unguja na Pemba.
Pia, alieleza juhudi za Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar ilivyoanza mradi wa ujenzi wa Vituo vya mafunzo ya Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa Vijana kwa Unguja na Pemba ambavyo vitachochea
maendeleo yao kwa kuitumia taaluma watakayoipata, ikiwemo kwenda sambamba na
Ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia.
Hata hivyo, Rais Dk. Mwinyi aliahidi kuanzishwa Sera mpya ya Maendeleo
ya Vijana itakayozingatia mahitaji ya wakati wa sasa na ujao, alitoa wito kwa
taasisi zote za Umma na binafsi, Washirika wa Maendeleo, Mabaraza ya Vijana, na
Asasi za Maendeleo ya Vijana, kushiriki kikamilifu kwenye utekelezaji wa Sera
hiyo kwa vitendo ili kufikia lengo lililokusudiwa na Serikali.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Habari,
Vijana Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita aliiahidi Serikali kuendeleza
fursa kwa vijana, kuwasimamia, kuratibu na kupunguza changamoto zinazowakabili.
Naye, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha
Mapinduzi, (UVCCM) Muhamed Kawaida, alipongeza juhudi za Serikali ya Dk. Mwinyi
kwa mara ya kwanza amefanikiwa kuwaweka pamoja vijana wa vyama vya mbalimbali bila
kujali tofauti za itikadi zao na kueleza kuwa hatua hiyo imeendelea kuimarisha
amani ya Zanzibar iliyopo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Vijana,
Yunus Juma Ali aliwaasa vijana kuendeleza heshima kwenye jamii, kuvumiliana na
kuyasema mambo yenye uhakika kwa kufanyia utafiti na kujiridhisha kabla ya
kuzungumza.
IDARA YA MAWASILIANO,
IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment