Alhaj Othman ametoa ukumbusho huo leo, mara tu baada ya Swala ya Ijumaa, alipojumuika na Waumini mbalimbali wa Kiislamu, katika Msikiti Mkuu wa Wete, Mkoa wa Kaskazini, Kisiwani Pemba.
Amefahamisha kuwa jamii zote na Nchi kwa ujumla, zinahitaji kudumu katika umoja, mshikamano na maridhiano, kama ilivyokuwa ikisisitizwa na Wazee hapo zamani, kupitia juhudi zao za malezi mema kwa watoto, sambamba na kuepuka mifarakano isiyokuwa na tija, licha ya tofauti ndogo ndogo, ambazo haziwezi kuepukika maishani.
“Kama si hivyo ilivyosisitizwa na wazazi wema hapo zamani, kupitia malezi mema ya watoto, leo hii tungelikosa hata watu wa kuongoza juhudi njema, zikiwemo za kusimamia na kuongoza Nyumba za Ibada”, amesema Mheshimiwa Othman.
Hivyo, pamoja na kushukuru juhudi za Ufadhili na Ujenzi Mpya wa Msikiti huo wa Asili katika Mji wa Wete, Mheshimiwa Othman ameihimiza jamii kuepuka kukhasimiana kwa sababu tu ya hitilafu na tofauti ndogo ndogo, ili maisha yaendelee katika hali bora ya mafanikio, na Nchi iendelee kubakia salama.
Naye, Khaatib na Imam wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa wa Wete, Sheikh Jamal Mohamed Abeid, amesema uzuri wa Dini ya Kiislamu ni kuhamasisha, Furaha, Kheri, Amani na Tabia Njema, ambapo miongoni mwa hizo ni kutekeleza ipasavyo amana na dhamana katika jamii.
Sheikh Jamal ameiasa jamii dhidi ya vitendo vya khiyana, udhalilishaji, rushwa, ukahaba na wizi wa mazao, vinavyoendelea kushamiri Nchini, akisema hivyo vinaleta karaha na kusababisha majozi na mwishowe hata maafa.
Katika kuhamasisha utekelezaji wa amana kisiwani hapo, Sheikh Jamal ambaye ni Mjumbe wa Baraza la Ulamaa Zanzibar, ameiomba Serikali kupigia-macho uzima na ubora wa Barabara ya Selem katika Mji wa Wete, kwa kuifanyia matengenezo, sambamba na kudhibiti mwendokasi wa vyombo vya moto, ikibidi hata kwa kuweka matuta, ili kuepusha hatari na ajali zisizokuwa za lazima.
Viongozi wa Kidini, Siasa na Watendaji wa Serikali wamejumuika Msikitini hapo, wakiwemo Maafisa- Wadhamini wa Wizara mbalimbali, akiwemo pia Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Bw. Salim Bimani.
Mheshimiwa Othman ambaye ameambatana na Mke wake, Mama Zainab Kombo Shaib, amewasili Kisiwani Pemba leo, kwa Ziara Maalum ya Siku 4 kwaajili ya Shughuli za Chama na Serikali.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Othman amefika na kuwajulia hali Wagonjwa na Wazee mbalimbali huko Wete, alipotembelea Familia zao, ambao ni pamoja na Maalim Rashid Hamad Othman, na Mzee Mohamed Haji Mohamed.
Kitengo cha Habari,
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,
Ijumaa, Septemba 15, 2023.
No comments:
Post a Comment