Habari za Punde

Mjadala wa Kitaifa wa Kuitangaza Zanzibar Kimichezo na Sanaa

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar Mhe.Tabia Maulidi Mwita amesema wameamuwa kuweka mikakati ya mageuzi ya kielimu ikiwemo michezo kupitia Wizara ya Elimu na mafunzo ya Amali Zanzibar.

Ameyasema hayo wakati wa mjadala  wa kitaifa wa kuitangaza Zanzibar kimichezo na  sanaa  huko ukumbi wa Madinatul Bahar.

Alisema mikakati hiyo itaweza kuwaibuwa vijana ambao wapo skuli na kujifunza michezo pamoja na sanaa na  kuwaendeleza wana michezo kwa  kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali.

Alisema Serikali kupitia Wizara ya Habari inaendeleza ilani na Sera ya Chama cha Mapinduzi kuhakikisha wanaibuwa vipaji  na kutengeneza miundo mbinu bora itakayowawezesha wana michezo na sanaa kushiriki kikamilifu mashindano ya kitaifa na kimataifa kwa nia ya kuitangaza Zanzibar kiutalii.

Pia alisema   atahakikisha michezo yote iliyokuwa haipo zanzibar kurudishwa  ikiwemo mchezo wa  marathon, mpira wa ufukweni (beach Soka) na mpira wa miguu wa wanawake ambao atawajengea misingi bora ya kuwawezesha kama vile vitendea kazi.

Rais wa ZFF Suleiman Mohammed Jabir amewataka wasanii na wana michezo kujifunza zaidi taaluma ya fani zao  pamoja na kuwacha kufanya kazi kwa  mazowea ili kuitangaza Zanzibar kiutalii na kimataifa.

Hata hivo, ameiomba Serikali kupitia Wizara kurudisha miradi iliyokuwepo ya awali ambayo itasaidia kuwasomesha makocha sehemu za nje kwa ajili ya kuwafundisha vijana na kuwa na makocha wa ndani ya nchi.

Mrajis wa Chama cha michezo Abubakar Lunda alisema awali michezo ilikuwa ni afya lakini kwa wakati huu michezo ni fursa ya kujipatia ajira na kukuza kipato.

Alisema kufundishwa kwa michezo katika ngazi za skuli haileti mzigo Bali inakuza vipaji na kupata ajira, hivyo ameitaka jamii kuwacha fikra za kuwa michezo inaleta mzigo kwa wanafunzi.

Mrajis wa Baraza la Sanaa  Sensa Filamu na Utamaduni BASSFU Juma  choum Juma  amefahamisha kuwa ni muhimu kufuata sheria zilizowekwa na Bassfu ili kuepuka makosa yanayojitokeza ya ukiukwaji wa sanaa na utamaduni nchini.

Nae Balozi wa Hakimiliki Africa Salum Maulid Stika  amewataka wasanii na wanamichezo kufanya sanaa ya utamaduni  kwa lengo la kuitangaza Zanzibar kiutalii na kupata pato lililokuwa na faida kwao.

Ameongeza kuwa ili wasanii na wana michezo wawe na sanaa nzuri ni vyema wakasaidia matatizo waliyokuwanayo ikiwemo changamoto ya mameneja ambao watakuza na kuimarisha tasnia ya sanaa na michezo hapa nchini.

Hata hivyo mdau wa sanaa Nd. Shamoun Hashim ameipongeza Wizara  ya Habari kwa juhudi kubwa wanazozichukuwa za kuhakikisha michezo na sanaa vinaimarika na kuwaunga mkono kwa kazi wanazozifanya na  kuamuwa kutowa shilingi Milioni kumi (10) kuwasomesha makocha watano ( 5 ) ili kuendeleza kazi za sana nchini.

Mjadala huo wa kitaifa uliwashirikisha pia wasani na wanamichezo kutoka sehemu mbalimbali ambao wanalengo la kuimarisha sekta ya sana na michezo hapa Zanzibar.



Washiriki wa mjadala  wa kitaifa wa kuitangaza Zanzibar kimichezo na  sanaa uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Madinatul Bahar Mbweni Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.