Habari za Punde

Ujio wa mvua za vuli, jamii yatakiwa kuwa na hadhari

 Na Khadija Khamis – Maelezo . 15/09/2023.

Jamii inatakiwa kuchukuwa tahadhari za mapema juu ya mvua za vuli zinazotarajiwa kuanza mwanzoni mwa Oktoba mwaka huu ili kujiepusha na athari zinazoweza kujitokeza ikiwemo mafuriko.

Hayo yameelezwa na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar Muhidini Ali Muhidini wakati wa kikao cha kujadili mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli   huko katika ukumbi wa Kamisheni hiyo, Maruhubi.

Amesema iko haja jamii kufuata muongozo wa elimu  ya mwenendo na mfumo wa mvua inayotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ili kujiandaa kuhama maeneo ya mabondeni mapema  jambo ambalo litasaidia kuwanusuru watu na mali zao.

Nae Mtaalamu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania(TMA) Hassan Khatibu Ameir amesema muelekeo wa mvua za vuli zinatarajiwa kuanzia wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Oktoba 2023 na kuisha wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Januari 2023.

Alifahamisha  kuwa athari zinazotarajiwa kujitokeza ni nyingi ikiwemo matukio ya mvua kubwa katika baadhi ya maeneo na kusababisha kutuwama kwa maji na mafuriko, hivyo iko haja ya Mabaraza ya Manispaa kuboresha mifumo ya kusafirishia maji taka ili kupunguza athari za  kutuama kwa maji na  mafuriko  .

Mtaalamu huyo alizitaka kamati za maafa katika ngazi za kijiji na wilaya kujiandaa kukabiliana na maafa hayo ili  kupunguza  athari pindi yatakapotokea.

Kwa upande wa Mtaalamu wa ICT Geography, (DRONE EXPERT ) Yussuf  Said Yussuf alifahamisha maafa na mifumo ya geografia ya Zanzibar  inaonyesha kuwa kuna baadhi ya watu wengi wanaishi  mabondeni jambo ambalo ni hatari wakati wa mvua kubwa .

“Uhalisia wa mambo watu hawatakiwi kujenga ndani ya mabonde wala njia kuu zinazopitisha maji ya mvua lakini  jamii haitaki kuyafahamu hayo .”alisema Mtaalamu Yussuf .

Aliyaeleza mabonde hatarishi hayo ni Mwantenga, ziwa, maboga, Jangamizini, Mto bomba, Mto Barafu, Mwera, Bitihamrani, Kwamtumwa Jeni Sebleni,  na mengine mengi ambayo kikawaida kutuwama maji .

Nao washiriki kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja, wameiyomba Mamlaka  ya Udhibiti wa Huduma ya Maji na Nishati (ZURA ) kupeleka nguvu za ziada kuyadhibiti mashimo ya mchanga yaliyomaliza kutoa huduma ndani ya maeneo yao ya  kaskazini ‘A’na Kaskazini ‘B’ ili yasiendelee kuleta adhari kwa wananchi hasa kipindi cha mvua kubwa .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.