Serikali kupitia
Ofisi ya Makamu wa Rais imesema itaendelea kushirikiana na vyombo vya habari
nchini katika kutoa wa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa uhifadhi na utunzaji wa
mazingira ikiwemo wa uhifadhi wa Tabaka la Ozoni.
Hayo yamesemwa
na Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Mitawi wakati
akifungua warsha ya mafunzo kwa waandishi wa vyombo vya habari kuhusu
udhibiti wa uingizaji wa kemikali
zinazodhibitiwa chini ya Itifaki ya Montreal iliyofanyika Septemba 16, 2023 jijini Dar es Salaam.
Mitawi
amesema Tanzania kama nchi nyingine Duniani imeendelea kuwa mstari wa mbele
katika kukabiliana athari za matumizi vifaa vya kemikali vyenye ukomo wa
matumizi kwa kuimarisha mifumo ya udhibiti wa kemikali hizo ambazo zinazodhibitiwa ambazo zina madhara mbalimbali katika jamii ikiwemo magonjwa,
ongezeko la joto duniani na mabadiliko ya tabianchi.
“Tutaendelea
kushirikiana na vyombo vya habari katika kuhakikisha elimu ya uhifadhi na
utunzaji wa mazingira inaifikia jamii…Tunatambua mchango mkubwa wa JET kwani
tangu kuanzishwa kwake mwaka 1991 imekuwa mstari wa mbele kuhamasisha jamii kutunza
na kuhifadhi mazingira” amesema Mitawi.
Akifafanua zaidi
Mitawi amesema ni takribani miaka 35 sasa tangu Jumuiya ya Kimataifa ipoamua
kuchukua hatua mahsusi za kunusuru tabaka la ozoni katika kulinda afya ya
binadamu na mazingira ambapo mwaka 1987 ilipitishwa Itifaki ya Montreal kuhusu
udhibiti wa kemikali zinazomong'onyoa tabaka hilo.
“Lengo kuu la
Itifaki hii ni kupunguza uzalishaji na matumizi ya kemikali zinazomong'onyoa
tabaka la Ozoni….Nafasi ya vyombo vya habari ni kubwa katika kuelimisha jamii
kuhusu athari ya matumizi ya kemikali hizi ambapo zimeleta athari mbalimbali
ikiwemo mabadiliko ya tabianchi” amesema Mitawi.
Amesema katika
jitihada za kuhifadhi tabaka la ozoni, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais
imeandaa na kutekeleza programu na shughuli mbalimbali ikiwemo kuendelea
kuhimiza jamii kupunguza shughuli za kibinadamu ambazo zinasababisha mabadiliko
ya tabianchi pamoja na kutoa mafunzo kwa Maafisa Forodha na
Wasimamizi wa Sheria maeneo ya mipakani.
Kwa upande wake,
Kaimu Mkurugenzi wa Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Kemilembe Mutasa
amesema juhudi mbalimbali zimeendelea kufanywa na Serikali katika Tabaka la
Ozoni ikiwemo amesema katika kuelekea Siku ya Tabaka la Hifadhi ya
Ozoni kutoa mafunzo kwa mafunzo mchundo na maafisa wa forodha na wasimamizi wa
sheria katika maeneo ya mipakani.
“Tanzania sio mzalishaji wa kemikali
hizi...Tumekuwa tukipokea kutoka nchi za nje..Tumeandaa kanuni, sera, sheria na
miongozo mbalimbali katika kuelimisha jamii na pia Tumekuwa na mfululizo wa
mafunzo haya kwa makundi mbalimbali ili kudhibiti kemikali hizi” amesema
Kemilembe.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo,
Bi. Mariam Mziwanda ameishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuandaa mafunzo
hayo na kutambua mchango wa vyombo vya habari katika kutoa elimu kuhusu
udhibiti wa tabaka la ozoni katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya
tabianchi.
“Suala la
usimamizi wa uhifadhi na utunzaji wa mazingira halipaswi kuachiwa Serikali pekee
…Ni wajibu wetu sote kuunga mkono juhudi hizo…Tunaishukuru Ofisi ya Makamu wa
Rais kutambua nafasi ya vyombo vya habari katika kufikisha elimu ya uhifadhi wa
tabaka la ozoni kwa jamii” amesema
Mariam.
Tarehe 16 Septemba kila mwaka, Tanzania huungana na Jumuiya ya Kimataifa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni . Kauli mbiu ya Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni mwaka 2023 ni “Hifadhi ya tabaka la ozoni na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi”
No comments:
Post a Comment