Habari za Punde

Kongamano la kwanza la mwaka la Mawakili na Maafisa sheria wa Serikali lafanyika Zanzibar

Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dkt. Mwinyi Talib Haji akifungua Kongamano la Mwaka la Mawakili na Maafisa Sheria wa Serikali katika Ukumbi wa Madinatul el- Bahri Mbweni, Zanzibar 

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Shaaban Ramadhan Abdalla akitoa neno la utangulizi la Kongamano la Mwaka la Mawakili na Maafisa Sheria wa Serikali katika Ukumbi wa Madinatul el- Bahri Mbweni, Zanzibar
Baadhi ya washiriki wa Kongamano la Mwaka la Mawakili na Maafisa Sheria wa Serikali wakifuatilia mada zilizokuwa zinawasilishwa huko katika Ukumbi wa Madinatul el- Bahri Mbweni, Zanzibar


Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dkt. Mwinyi Talib Haji (wa kati kati waliokaa) akiwa katika Picha ya pamoja Baadhi ya washiriki wa Kongamano la Mwaka la Mawakili na Maafisa Sheria wa Serikali huko katika Ukumbi wa Madinatul el- Bahri Mbweni, Zanzibar
 Na Faki Mjaka-Afisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar 01.10 2023

 

Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dk. Mwinyi Talib Haji amewaasa Mawakili na Maafisa Sheria wa Serikali kuacha kufanya mambo yanayokatazwa na Sheria za maadili na ambayo yatapelekea mgongano wa maslahi katika kazi zao.

 

Dk. Mwinyi ameyasema hayo wakati akifungua Kongamano la kwanza la  mwaka la Mawakili na Maafisa sheria wa Serikali lililofanyika katika ukumbi wa hotel ya Madinat al-bahr Mbweni, Zanzibar.

 

Amefahamisha kuwa, mfanyakazi anapokuwa Wakili wa Serikali au Afisa Sheria hutakiwa kuacha kufanya kazi binafsi za uwakili ikijumuisha kuandaa kazi za kisheria pamoja na kuwawakilisha wateja mahakamani kwa malipo.

 

Amesema maadili ni muhimu katika utendaji wa kazi zao za kila siku na kwamba, bila kuzingatia maadili kuna uwezekano mkubwa wa kupelekea mgongano mkubwa wa maslahi katika utendaji wa kazi.

 

“Hakuna Kada isiyokuwa na maadili, na kwa wanasheria wa Serikali maadili yanagusa mfumo mzima wa Maisha ya kila siku hivyo, tujitahidi kufanya kazi zetu kwa umahiri na uaminifu mkubwa” alinasihi Mwanasheria Mkuu.

 

Pamoja na kuwasisitiza wataalam hao kufuata maadili, Mwanasheria Mkuu huyo wa Zanzibar amewanawasihi kuendeleza ushirikiano miongoni mwao kwani kupitia ushirikiano wa pamoja, itawarahisishia kutatua changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.

 

Amefahamisha kuwa ushirikiano utakapoimarika na kila mmoja kuwajibika ipasavyo itakuwa rahisi kutimiza ndoto na malengo ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi katika kudumisha amani wakati wote na kuchochea ukuzaji wa uchumi wa nchi na ustawi bora wa jamii.

 

Dk. Mwinyi amewaahidi Mawakili na Maafisa sheria kuwa, Afisi yake inatarajia kufanya Mkutano kama huo na Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi mbali mbali za Serikali kwa lengo la kujadiliana zaidi ili Mawakili na Maafisa sheria hao waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

 

“Nataka nikuahidini ndugu zangu kuwa, tunatarajia kufanya Mkutano na Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi mbali mbali za Serikali ili tuwakumbushe umuhimu wenu na namna bora ya kushirikishwa katika taasisi zenu hasa kwenye eneo la Mikataba kwa faida ya Taasisi na Serikali kwa ujumla” aliahidi Dk. Mwinyi.

 

Aliwataka kutilia maanani mada zilizowasilishwa na Wataalamu kwani zote zina umuhimu mkubwa katika kujengea uwezo zaidi wa utekelezaji bora wa majukumu ya kila siku.

 

Akiwasilisha Mada kuhusu Usimamizi wa Mikataba Mhandisi Ali Said kutoka Mamlaka ya uhifadhi na uendelezaji wa Mji Mkongwe Zanzibar aliwakumbusha Mawakili na Maafisa sheria wajibu wa kila mmoja kushiriki kikamilifu katika kuandaa, kuipitia na kutoa ushauri wa kisheria katika Mikataba hiyo ili kuifanya iwe na tija kwa Serikali na taifa kwa ujumla.

 

Akiwasilisha Mada inayohusiana na Mahusiano baina ya Mawakili na Maafisa Sheria wa Serikali kutoka Afisi ya Mwanasheria Mkuu na Taasisi nyengine, Wakili kutoka Afisi ya Mwanasheria Mkuu Hamisa Mmanga ina amesema lengo la mada hiyo ni kukumbushana kuhusiana na kazi za Afisi ya Mwanasheria Mkuu na umuhimu wa uwepo wa mahusiano mazuri baina yao ambayo yatapelekea ufanisi katika utekelezaji wa majukumu.

 

Kwa upande wao Mawakili na Maafisa sheria walielezea changamoto wanazokumbana nazo katika baadhi ya Ofisi ikiwemo kutokushirikishwa kikamilifu, kutokupandishwa madaraja na maslahi duni ambayo kwa kiasi kikubwa yanarudisha ari ya utendaji wao wa kazi.

 

Akitoa neno la shukran kwa niaba ya wenzake Mwanasheria kutoka Wizara ya Fedha Hussein Migoda alitoa wito kwa Afisi ya Mwanasheria Mkuu kuhakikisha makongamano hayo yanakuwa endelevu na yashirikishe wadau wengi zaidi ili wapate kujifunza.

 

Aidha Migoda aliishukuru Afisi hiyo kwa kuandaa Kongamano hilo hasa kwa kuzingatia kuwa watalitumia kama sehemu ya kuwasilisha changamoto zinazowakabili katika utendajikazi wao wa kila siku kwa lengo la kupatiwa ufumbuzi.

 

Akifunga Kongamano hilo la siku moja Naibu Mwanasheria Mkuu Zanzibar Shaaban Ramadhan Abdalla aliishukuru Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora pamoja na wafadhili wa Kongamano hilo ambao ni Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwa ushirikiano uliofanikisha Kongamano hilo.

 

Aidha aliahidi kuzifanyia kazi changamoto zilizowasilishwa na Mawakili pamoja na Maafisa sheria wa Serikali huku akiahidi kuwa watajitahidi kuliimarisha Kongamano hilo ili liweze kuleta tija zaidi kwa maslahi ya Wanasheria na Taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.