Habari za Punde

Mhe Hemed aendelea na ziara yake ya kukagua uhai wa chama Wilayani Lushoto

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu. Hemed Suleiman Abdulla ambaye ni Mlezi wa CCM Mkoa wa Tanga Akisalimiana na Viongozi na wanachama wa CCM Wilaya ya Lushoto mara baada ya kuwasili katika ukumbi wa CCM Wilaya ya Lushoto ikiwa ni muendelezo wa Ziara yake ya Kuimarisha Chama cha Mapinduzi kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu. Hemed Suleiman Abdulla ambaye ni Mlezi wa CCM Mkoa wa Tanga Akizungumza na Viongozi na Wanachama wa CCM katika Ukumbi wa CCM Wilaya ya Lushoto ikiwa ni muendelezo wa Ziara yake ya Kuimarisha Chama cha Mapinduzi kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu Hemed Suleiman Abdulla ameridhishwa na uimara wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Tanga hatua ambayo inaleta matumaini kwa CCM kushinda katika Chaguzi zote zijazo.

Mhe. Hemed ambae ni Mlezi wa CCM Mkoa wa Tanga ameyasema hayo kwa nyakati tofauti alipokuwa akizungumza na Viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Lushoto na Wilaya ya Korogwe akiendelea na ziara yake ya kuimarisha Chama Mkoa wa Tanga.

Amesema kuimarika kwa CCM Mkoani Tanga kunatokana na Miongozo inayotolewa na Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samua Suluhu Hassan anayoitoa kwa Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi.

Amesema ana Imani Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Tanga kitashinda katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 hatua ambayo itatoa matumaini makubwa kushinda Uchaguzi Mkuu wa Dola ifikapo 2025.

Amefarijika kuona ziara za Viongozi wa Mkoa na Wilaya zinafanyika mara kwa mara pamoja Vikao vya Kikatiba na kuwataka Viongozi kushuka kwa wanaowaongoza ili kujua changamoto zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi hatua itakayoongeza Imani ya wananchi kwa  CCM na Serikali yao.

Mhe. Hemed ambae ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Serikali imesogeza miradi mingi ya maendeleo kwa wananchi wake ili kupata huduma bila ya kujali itikadi za wananchi.

Aidha amefahamisha kuwa Serikali itaendelea kuulinda na kuudumisha Muungano ambapo ndani ya muda mchache tayari hoja kadhaa za Muungano zimeshapatiwa ufumbuzi na siku chache zijazo Kamati inakwenda kumaliza hoja zilizobakia ili wananchi waendelee kunufaika na uwepo wa Muungano huo.

Nae Mjumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Tanga na Mwenyekiti wa Umoja wa wanawake Mkoa huo Ndg.  Al - Shaymaa John Kwegyir ameeleza kuwa UWT inaendelea na ziara za mara kwa mara kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka  2020-2025 pamoja na kuhubiri mambo mazuri yaliyofanywa na Serikali  katika Mkoa huo.

Aidha amesema wameweza kuwafikia wazazi na walezi na Kushajihisha kusimamia malezi mazuri kwa watoto ili kumaliza janga la mpromoko wa maadili ambalo humaliza nguvu kazi ya Taifa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Lushoto Ndg Ali Salum Dafa ameeleza kuwa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Lushoto kimeendelea kuimarisha Chama kwa ziara za mara kwa mara, kukaa vikao vya kikatiba pamoja na kuboresha Miradi ya Chama hatua ambayo inadhihirisha ushindi wa CCM katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na Uchaguzi wa Dola mwaka 2025.

Amesema maendeleo yanayoendelea kupatikana Mkoa wa Tanga yanatokana na mashirikiano yaliyopo baina ya Uongozi wa CCM Mkoa wa Tanga na Wilaya zote pamoja na Serikali ya Mkoa na za Wilaya kuamua kufanya majukumu yao kwa pamoja hatua ambayo inaongeza kasi ya uwajibika kwa watendaji wa Chama na Serikali katika kuwatumikia watanzania.

Abdulrahim Khamis

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

12 /10/ 2023

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.