Habari za Punde

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Mlezi wa CCM Mkoa wa Tanga Mhe.Hemed Suleiman Abdulla Akiendelea na Ziara Yake Wilaya ya Mkinga na Tanga Mjini

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu Hemed Suleiman Abdulla ambaye ni Mlezi wa CCM Mkoa wa Tanga akizungumza na Viongozi na wanachama wa CCM wa Wilaya ya Mkinga katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga ikiwa ni muendelezo wa Ziara ya Kuimarisha Chama kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewataka Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi Mkoani Tanga kudumisha umoja na mshikamani ndani ya Chama hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka 2024.

Akizungumza na Viongozi mbali mbali wa CCM  wa Wilaya ya Mkinga na Wilaya ya Tanga Mjini Mhe. Hemed ambae pia ni Mlezi wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Tanga amesema kuwepo kwa umoja, mshikamano, upendo na haki kwa Viongozi na Wanachama wa CCM Mkoani humo ndio silaha kubwa ya kuwashinda wapinzani katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka 2024.

Amefahamisha kuwa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ametekeleza miradi Mingi ya maendeleo katika Mkoa wa Tanga hivyo, wana CCM wanapaswa kuhakikisha CCM inashinda katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na isitokee hata kitingoji kimoja kikachukuliwa na Wapinzani.

Mhe. Hemed amesisitiza suala la nidhamu ndani ya Chama na kuachana na tabia ya kuchafuana, majungu na matabaka ambayo yanaleta mpasuko mkubwa na kukizorotesha Chama katika kuwaletea maendelo Wananchi.

Amewataka Viongozi wa CCM kutekeleza majukumu yao na ahadi zao walizoziahidi wakati wanaomba ridhaa za kuwa Viongozi sambamba na kufanya  ziara kuweza kuwafikia wananchi ili kutambua changamoto zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi jambo ambalo litachochea kasi na maendeleo kuanzia Vitongoji hadi Taifa.

Amezitaka Kamati za Siasa na Kamati Tekelezaji za Jumuiya za Chama kuhakikisha wanazidisha umoja na mshikamano katika kukitumikia Chama ili kukivusha salama katika chaguzi zote zijazo.

Amesema maendeleo yanayoletwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yanatoka na uwepo wa Amani na utulivu hivyo, ni wajibu kuendelea kuilinda na kuidumisha amani iliyopo  kwa maslahi ya watanzania.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ametoa onyo kwa wale wote walioanza kutangaza nia ya kugombea nafasi mbali mbali za Uoongozi na kusema kuwa muda wa kufanya hivyo haujafika na yoyote atakaebainika Chama hakitasita kumchukulia hatua za kinidhamu.

Nae Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kutoka Mkoa wa Tanga Ndg. Muhamed Salum Ratko ameeleza kuwa ni wajibu wa wanachama na Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi kuutumia  muda huu kuzidi kuimarisha Chama ili kushinda katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu wa Dola wa mwaka 2025.

Amesema ili kushinda uchaguzi ni lazima kuunganisha nguvu kuanzia ngazi ya Shina hadi Mkoa ili kuongeza Imani ya wananchi kwa CCM na Serikali yao.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Waziri Kindamba ameeleza kuwa Serikali ya Mkoa tayari imeshaanza kutafuta wawekezaji kuwekeza katika ukanda wa Bahari ili kukuz uchumi wa Taifa na wa Mtu mmoja mmoja kupitia fursa zinazopatikana katika ukanda huo.

Aidha amesema kwa kuwa Sekta ya utalii ni miongoni mwa sekta zinazonufaisha Mkoa huo Serikali ya Mkoa tayari imeshaanza kuzungumza na wadau ili kuelekeza nguvu zao katika sekta hiyo.

Kwa upande wake Mbunge wa Mkinga na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula ameeleza kuwa Wizara imetatua changamoto ya Tembo kuingia katika maeneo ya Kilimo na kuharibu mimea na mazao katika Kijiji cha Mazoga  ambapo Wizara inaendelea kuwapatia elimu wananchi kujua namna ya kukabiliana na Wanyama hao.

Katika ziara hiyo Mlezi wa CCM Mkoa wa Tanga Ndg. Hemed Suleiman Abdulla amekabidhi jumla ya Shilingi Milioni Tano na Laki Sita kwa ununuzi wa Mabati ya Ofisi ya CCM Wilaya ya Mkinga inayotarajiwa kukamilika ujenzi wake Mwishoni mwa mwaka huu.Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Ndugu Hemed Suleiman Abdulla ambaye ni Mlezi wa CCM Mkoa wa Tanga amewasili Wilaya ya Mkinga na kupokea Taarifa ya utekelezaji ya CCM Wilaya ya Mkinga ikiwa ni muendelezo wa Ziara yake ya  Kuimarisha Chama katika kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.