Habari za Punde

Tanzania yakipigia chapuo kiswahili kutumika mikutano ya Benki ya Dunia na IMF

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum (kushoto), ambaye anaongoza Ujumbe wa Tanzania katika Mikutano ya Mwaka ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), inayofanyika Marrakech, nchini Morocco, kwa niaba ya Waziri wa Fedha wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, ambaye pia ni Gavana mbadala wa Tanzania katika Benki ya Dunia, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, wakielekea kwenye Mkutano wa 26 wa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu kutoka Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika ambazo ni wanachama wa Benki ya Dunia, ambapo aliwasilisha ombi la Tanzania la kutaka Benki hiyo kukifanya kiswahili kuwa miongoni wa lugha ya mawasiliano wakati wa mikutano yake kutokana na kukua kwa lugha hiyo na kutumika kwenye mikutano mingine ya Kikanda na Kimataifa. 
 

Na Benny Mwaipaja, Marrakech

Tanzania imeishauri Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kukifanya kiswahili kuwa miongoni wa lugha za mawasiliano wakati wa mikutano yake kutokana na kukua kwa lugha hiyo na kutumika kwenye mikutano mingine mingi ya Kikanda na Kimataifa.

Ushauri huo umetolewa Mjini Marrakesh nchini Morocco, na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, wakati wa Mkutano wa 26 wa Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu kutoka Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika ambazo ni wanachama wa Benki ya Dunia.

Dkt. Saada Mkuya Salum, anayeongoza ujumbe wa Tanzania katika Mikutano ya Mwaka ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), kwa niaba ya Waziri wa Fedha wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alisema kuwa ni wakati muafaka wa kukijumuisha Kiswahili katika mijadala ya Taasisi hizo kubwa za Fedha duniani kwa kuwa wanachama wake wengi kutoka katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, wanazungumza lugha hiyo.

“Takribani watu milioni 200 wanazungumza Kiswahili duniani, tumewasilisha ombi hili ikiwa ni jitihada za Serikali za kukibidhaisha Kiswahili saw ana lugha nyingine zinazotumika kama lugha rasmi kwenye mikutano ya Benki ya Dunia na IMF), alisema Dkt. Saada Mkuya Salum

Agenda hiyo itajadiliwa wakati wa Mkutano wa 27 wa Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika ambazo ni wanachama wa Benki ya Dunia, wakati wa Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), itakayofanyika Washington D.C, nchini Marekani, Mwezi Aprili, Mwakani.

Aidha, katika mkutano huo wa 26 wa Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika, wajumbe waliiomba Benki ya Dunia kutoa fedha kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi kwa kuwezeha biashara ya hewa ukaa, kusaidia bajeti za nchi wanachama na kuongeza kiwango cha fedha za mikopo nafuu na misaada kwa nchi zinazoendelea kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Waliitaka pia Benki hiyo kuzihudumia nchi wanachama wake kwa usawa wakati wa majanga ikiwemo matatizo ya mizozo ya kivita kama wanavyofanya kwenye nchi nyingine zenye matatizo kama hayo kwenye mabara mengine, hatua inayokwamisha juhudi za nchi hizo kukabiliana na changamoto hizo na kukwamisha juhudi za kujikwamua kiuchumi.

Mkutano huo umehudhuriwa pia na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, ambaye pia ni Gavana mbadala wa Tanzania katika Benki ya Dunia, na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamisi Shaaban.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.