Habari za Punde

SADC Mguu Sawa Kupeleka Misheni ya Ulunzi wa Amani Nchini DRC

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akiwa na Rais wa Afrika Kusini Mhe. Cyril Ramaphosa (kushoto) Rais wa Zambia Mhe. Hakainde Hichilema (kulia) katika picha ya moja muda mfupi kabla ya kuanza kwa  Mkutano wa dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika SADC jijini Luanda, Angola
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika picha ya pamoja na Rais wa Afrika Kusini Mhe. Cyril Ramaphosa, Rais wa Zambia Mhe. Hakainde Hichilema, Rais wa Angola Mhe. João Lourenço, Rais wa Zimbabwe Mhe. Emmerson Mnangagwa pamoja na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Félix Tshisekedi pamoja na Viongozi mbalimbali kabla ya kuanza kwa Mkutano wa dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika SADC, jijini Luanda, Angola 


Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wameazimia kupeleka Misheni ya Ulinzi wa Amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (SAMIDRC) kushughulikia masuala muhimu yanayoathiri utulivu na amani nchini humo kufuatia mapigano ya muda mrefu baina ya makundi ya waasi yenye silaha. 

 

Azimio hilo limefikiwa kwenye Mkutano wa dharura wa Wakuu wa nchi na Serikali wa SADC uliofanyika jijini Luanda, Angola tarehe 04 Novemba 2023. 

 

Awali akizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano huo Rais wa Angola Mheshimiwa João Manuel Gonçalves Lourenço na Mwenyekiti wa SADC alieleza kuwa sasa ni wakati muafaka wa kanda hiyo kuhakikisha kuwa DRC inapata amani na utulivu ambao imeukosa kwa muda mrefu huku ukisababisha vifo vya watu wasio na hatia, familia kufarakana kwa kukimbia machafuko na uharibifu wa mali, hivyo kuwakosesha wananchi nafasi ya kujiletea maendeleo yao na ya kizazi kijacho. 

 

“Mkutano huu ni muhimu kwa kuwa unaenda kuweka juhudi za pamoja za nchi wanachama wa SADC katika kuleta mabadiliko chanya nchini DRC, ni imani yangu maamuzi yetu yanaenda kuamua mustakabali mwema wa ndugu zetu wa DRC na kuleta matumaini mapya kwa mamilioni ya watu ambao kwa muda mrefu wamekuwa na uhitaji wa utulivu na amani ya kudumu” Alisema Rais Lourenço.

 

Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, akizingumza katika Mkutano huo ameeleza kuridhishwa kwake na namna Jumuiya hiyo inavyothamini umuhimu wa kuimarisha hali ya ulinzi na usalama, na kuongeza kuwa hatua hiyo ni uthibitisho tosha wa kwamba kanda inaenzi misingi na malengo ya kuanzishwa kwake. 

 

Kwa upande wake Rais wa Zambia Mheshimiwa Hakainde Hichilema ambaye pia ni mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (Organ Troika) akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano wa kilele wa Asasi hiyo uliofanyika awali, alieleza kuwa kuimarika kwa usalama wa DRC kutaleta tija katika eneo lote la Kusini mwa Afrika na Afrika kwa ujumla wake. 

 

“Tunaamini kuwa DRC imara na salama itachangia katika ustawi wa amani ya kikanda na kuchochea maendeleo ya kiuchumi hivyo, tukiwa kama wanachama wa SADC tunasukumwa na dhamira hiyo ya kutafuta amani na utulivu wa nchini DRC” Alisema Rais Hichilema

 

Katika hatua nyingine mkutano huo wa Wakuu wa Nchi umetoa wito kwa mashirika yanayojihusisha na utoaji wa misaada mbalimbali ya kibinadamu kuendelea kutoa mahitaji muhimu kwa raia wa DRC wanaothiriwa na machafuko yanayoendelea nchini humo ikiwemo chakula, malazi na matibabu. 

 

Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliohudhuriwa na nchi 12 umehitimishwa leo Novemba 4, 2023 jiijini Luanda, Angola.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.