Habari za Punde

Mabalozi Wapongeza Juhudi za Serikali Uokoaji wa Wananchi Hanang,Waahidi Misaada Zaidi ya Kibinadamu

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akizungumza na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika wa Kimataifa Jijini Dar es Salaam alipokutana nao na kuwaelezea kilichotokea Hanang mkoani Manyara na hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na janga hilo

Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa nchini wamepongeza jitihada zinazochukuliwa na Serikali katika zoezi la uokoaji Hanang, kutokana na maporomoko ya tope kutoka katika mlima Hanang kufuatia mvua kubwa iliyonyesha Mkoani Manyara tarehe 02 Disemba, 2023.

Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika hayo wametoa pongezi hizo Jijini Dar es Salaam walipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) aliyewaita kuwaelezea kilichotokea Hanang mkoani Manyara na hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na janga hilo.

Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Waziri Makamba amesema maporomoko hayo ya tope yamesababisha vifo vya watu 72, kujeruhi watu 117, kuharibu mali za watu, makazi na miundombinu ya barabara, maji na umeme.

“Serikali ya Tanzania inaishukuru Jumuiya ya Kimataifa nchini kwa jinsi ilivyoikimbilia na kusaidia wahanga wa maporomoko hayo hasa katika kusaidia urejeshaji wa huduma za muhimu za kibinadamu kwa wananchi wa Katesh” alisema.

Amesema katika kukabiliana na janga hilo, Serikali iliunda Kamati ya Kitaifa ya Maafa iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshirikiana na mamlaka ya Mkoa wa Manyara na kufungua akaunti Maalum ya maafa kwa ajili ya kuratibu na upokeaji misaada mbalimbali ili kusaidia wahanga wa maporomoko hayo na kuwezesha maisha ya watu kuendelea kama kawaida.

“Wahanga bado wanahitaji misaada ya kibinadamu ya hali na mali, wengi wamepoteza makazi yao na kupoteza wapendwa wao pamoja na kuharibika kwa miundombinu ya barabara, maji na umeme na kusababisha maisha kusimama katika eneo hilo” alisema.

Amesema Serikali imeandaa maeneo maalum kwa ajili ya kuwahifadhi na kuwahudumia wahanga kwa kuwapatia huduma muhimu za kibinadamu, kuwatibu majeruhi, na kuwaokoa na kuwaondoa watu katika maeneo yaliyoathiriwa.

Amesema Serikali inaendelea na zoezi la kutafuta miili ya watu katika matope, kuhudumia shughuli za mazishi ya watu waliofariki na kuwafariji watu waliopoteza wapendwa wao kutokana na maporomoko hayo ili waweze kurejea katika hali zao za kawaida.

Naye Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Bw. Zlatan Milišić amepongeza hatua za haraka zilizochukuliwa na Serikali katika zoezi la uokoaji wa wananchi na mali zao huko Hanang na kuongeza kuwa Ofisi ya Umoja wa Mataifa Tanzania itaendelea kushirikiana na Serikali na kwamba Mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini yameungana na kuchanga misaada ya yao ya kibinadamu kwa ajili ya kusaidia wahanga hao ambayo wataikabidhi kwa Serikali.

Balozi wa Kenya amesema Kenya kama nchi jirani iko pamoja na Watanzania katika sala na maombi kuwaombea marehemu na kutoa pole kwa familia za marehemu

Akizungumza katika kikao hicho Balozi wa Somalia nchini Mhe. Zahra Ali Hassan amesema Umoja wa Mabalozi wa Afrika kwa umoja wao wameungana na kuwaingiza katika maombi wahanga wa maporomoko hayo na kuchanga misaada ya kibinadamu ambayo wataikabidhi kwa Serikali na kutoa pole kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Watanzania wote kwa maafa hayo makubwa yaliyotokea nchini.

Balozi wa Msumbiji Mhe.  Ricardo Mtumbuida amesema Msumbiji inaungana na Tanzania na kutoa pole kwa Mhe. Rais, Watanzania na wahanga wote na kuwaombea marehemu wapumzike kwa amani.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akizungumza na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika wa Kimataifa Jijini Dar es Salaam alipokutana nao na kuwaelezea kilichotokea Hanang mkoani Manyara na hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na janga hilo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba (Mb.) akizungumza na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika wa Kimataifa (hawapo pichani) Jijini Dar es Salaam alipokutana nao na kuwaelezea kilichotokea Hanang mkoani Manyara na hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na janga hilo
Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Bw. Zlatan Milišić akichangia jambo wakati wa kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika wa Kimataifa Jijini Dar es Salaam ambapo Waziri Makamba aliwaelezea kilichotokea Hanang mkoani Manyara na hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na janga hilo
Balozi wa Somalia nchini, Mhe. Zahra Ali Hassan akichangia jambo wakati wa kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika wa Kimataifa Jijini Dar es Salaam ambapo Waziri Makamba aliwaelezea kilichotokea Hanang mkoani Manyara na hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na janga hilo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.