Habari za Punde

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Ameifungua Barabara ya Kiwango cha Lami ya Kipapo hadi Mgelema Mkoa wa Kusini Pemba

 

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman akikata utepe kuifungua Barabara ya Kipapo hadi Mgelema Mkoa wa Kusini Pemba, ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na (kulia kwake) Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Mhe.Dkt. Khalid Salum Mohammed. 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman akiondoa poazia kuweka jiwe la msingi la ufunguzi wa Barabara ya Kipapo hadi Mgelema Mkoa wa Kusini Pemba, ikiwa ni shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar 

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amesema kwamba kujengwa kwa Barabara ya Kipapo -Mgelema mkoa wa kusini Pemba kutasaidia kuondosha changamoto kubwa ya tatizo la usafiri kwa wananchi wa maeneo hayo na kuwataka waitumie Zaidi kwa manufaa ya kiuchumi .

Mhe. Othman ameyasema hayo alipozungunza katika ufunguzi wa Barabara ya Kipapo- Mgelema wilaya ya Chake chake Pemba  ikiwa ni shamra shamra za sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar kutimia miaka 60.

Amesema kutokana na juhudi za serikali kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo kwa awamu ya kwanza yenye urefu wa kilomita 5.3 kutawawezesha wakulima kusafirisha mazao yao kwa urahisi na  kuwepo unafuu wa gharama kwa wananchi wa maeneo hayo.

Aidha amesema kwamba hatua hiyo pia itawasaidia wananchi kuzifikia kwa wepesi huduma mbali mbali ikiwemo elimu na Afya sambamba na unafuu wa usafiri wa abiria .

Mhe. Makamu amewataka wananchi  wakaazi waliopitiwa na Barabara hiyo kuhakikisha kwamba wanaitumia kwa maslahi ya kiuchumi ikiwa ili kusaidia kukuza maendeleo yao hasa katika sekta za kilimo na biashara.

Sambamba na hayo Mhe. Othman amewakumbusha wananchi hao kuendelea kutunza mazingira kwa kupanda miti ya uchumi na matunda pamoja na mengineyo kwa kuwa kufanya hivyo kutawasaidia kiuchumi.

Mhe. Othman ameongeza kwamba jitihada  za ujenzi wa barabara pia zitawawezesha wananchi kujishughulisha kwa wepesi na shughuli za biashara mbali mbali na kuweza kupata kipato jambo litakalochangia kupunguza umasikini kwa wananchi hao ikiwa ndio  faida ya Mapinduzi ya mwaka  1964.

Amefahamisha wananchi hao kwamba ujenzi wa barabara unagharama kubwa ambapo kwa makisio ya chini kilomita moja hujengwa kwa wastani wa dola laki sita za Marekani ambazo ni Zaidi ya shilingi bilioni 1.3 za Tanzania .

Hivyo, amewataka wananchi kuzithamni juhudi hizo za serikali kwa kila mmoja kutimiza wajibu katika kuzitunza na pia kuzingatia matumizi sahihi ya barabara ili ziendelee kudumu na kuwanufaisha Zaidi wananchi.

Kutokana na hatua hiyo ameitaka  wizara ya Ujenzi  Mawasiliano na uchukuzi Zanzibar kuhakikisha wanatoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya barabara.

Amesema kwamba serikali kwa kuwathamini wananchi wake tayari imetumia Zaidi ya shilingi milini mia tano na sabiini na mbili kuwalipa fiadia wananchi ambao mashamba na nyumba na zao  yao yameathirika kutokana na kupitia na ujenzi wa barabara hiyo.

Akizungunzia suala la janga la udhalilishaji Mhe. Othman amewataka wananchi wote kushiriki katika mapambano hayo lakini pia kuacha tabia iliyozuka kwa baadhi ya watu kulifanya suala la udhalilishaji kwamba ni biashara na kuwabambikizia kesi wananchi wasiohusika na masuala hayo.

Naye Waziri wa Mawasiliano na usafirishaji Zanzibar Dk. Khalid Salum Abdalla amesema amesema kwamba chachu ya maendeleo ya kiuchumi ni kuwepo miundombinu bora ikiwemo ya barabara na viwanja vya ndege na kwamba serikali ya mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikitilia maanani sana suala hilo katika jitihada za kukuza uchumi na maendeleo kwa wananchi  wa Unguja na Pemba.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Matar Zahor Masoud amesema kwamba ujenzi wa barabara hiyo ni hatua muhimu ya wananchi wa eneo hilo kuwezeshwa kiuchumi na kwamba Zaidi ya nusu ya karafuu zote zinazozalishwa Pemba zinatoka katika mkoa wa Kusini na eneo hilo likiwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa zao la karafu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo  Bi Khadija Khamis Rajab amesema kwamba barabara hiyo inauwezo wa kupita magari yenye uzito usiozidi tani kumi na kwamba wananchi wote wanao wajibu wa kuhakikisha kwamba wanaitunza barabara hiyo  ili iweze kudumu .

Mwisho .

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar kupitia Kitengo chake cha Habari leo tarehe 28.12.2023.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.