Habari za Punde

ZAWEMA na WMA Watiliana Saini Mashirikiano ya Kiutendaji

Katibu Mkuu wizara ya  Biashara na maendeleo ya Viwanada SMZ  (kushoto)  Ali Khamis Juma na katibu mkuu wizara  ya viwanda na Biashara SMT  Dkt.Hashil Abdalla  wakishuhudia  utiaji wa saini hati ya makubaliano ya ushirikiano wa kiutendaji kati ya Wakala wa vipomo wa Tanzania bara na Zanzibar  katika Mkutano wa wakuu wa taasisi za SMZ na SMT uliofanyika ukumbi wa Dkt. Hussein Mwinyi kituo cha maonesho ya Biashara Nyamanzi katika kusherehekea miaka 60 ya Mapinduzi. 

Na Rahma Khamis Maelezo Zanzibar.

Wakala wa vipimo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wametiliana  saini hati ya makubaliano ya ushirikiano   ili kuimarisha utendaji kazi wao. 

 

Akizungumza mara baada ya kushuhudia utiaji saini huo huko  Ukumbi wa Dokt Mwinyi kituo cha maonesho ya biashara Nyamanzi Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara SMT  Dkt. Hashil Abdalla amesema  ni vyema kuimarisha mashirikiano kati ya taasisi hizo ili  kuhakikisha vipimo vyote na thamani ya fedha inamfikia mtumiaji kwa usahihi.

 

 Amesema, kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo Wakala wa Vipimo ndio taasisi pekee inayopaswa kusimamia matumizi sahihi ya vipimo kwa kuhakikisha kuwa vipimo vinavyotumika katika biashara viko sahihi, na kuzingatia matumizi sahihi ya vipimo ili kuepusha madhara yatokanayo na vipimo batili na  kulinda walaji na watumiaji.

 

Aidha amesema makubaliano hayo yatasaidia  kuimarisha utendaji wa kazi na kuongeza ufanisi utakaopelekea kufikia malengo ya  Taasisi hizo.

 

Mkurugenzi wa wakala wa Vipimo Zanzibar ZAWEMA Mohammed Simai Mwalim ameeleza kuwa endapo vipimo vitasimamiwa kwa usahihi katika  bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini na bidhaa zinazoingizwa kutoka nje ya nchi itasaidia Serikali kukusanya kodi kwa usahihi .

 

Hata hivyo alisema  endapo  vipimo hivyo havitasimamiwa vyema  itasababisha wananchi kupata  kupata huduma au bidhaa ambazo haziendani na thamani ya fedha wanayotumia.

 

Mkurugenzi Mohammed alitoa wito kwa wananchi na wafanyabiashara wote wa Tanzania bara na Zanzibar kuhakikisha wanatumia vipimo sahihi na endapo watakutana na changamoto yoyote inayohusu vipimo wafike kwenye ofisi za Wakala wa Vipimo kwa ajili ya kupata msaada wa kitaalamu.

 

Hata hivyo aliwaonya Wamiliki wa vipimo  kutochezea vipimo kwa lengo la kuwaibia wananchi, kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kufanya vitendo hivyo ambavyo vinakatazwa hata kwenye maandiko matakatifu.

 

Nao Washiriki walioshuhudia utiaji wa saini huo walisema kuwa makubaliano hayo yametiwa saini katika kipindi muafaka cha  kuadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi na yataongeza mashirikiano zaidi ili kuyaenzi na kuyalinda Mapinduzi hayo.

 

Hati hiyo ya makubaliano ya kiutendaji  yalisainiwa na Mtendaji Mkuu  wakala wa vipimo Bara (WMA) Stela  Kahwa na  kwa upande wa Zanzibar Mkurugenzi wakala wa vipimo Zanzibar ZAWEMA Mohammed Mwalim Simai.




Katibu Mkuu wizara ya  viwanda na Biashara SMT Dkt.Hashil Abdalla  akizungumza mara baada ya kushuhudia utiaji wa saini hati ya makubaliano ya ushirikiano wa kiutendaji kati ya Wakala wa vipomo wa Tanzania bara na Zanzibar  katika Mkutano wa wakuu wa taasisi za SMZ na SMT uliofanyika ukumbi wa Dkt. Hussein Mwinyi kituo cha maonesho ya Biashara Nyamanzi katika kusherehekea miaka 60 ya Mapinduzi. 

PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.