Habari za Punde

Wajasiriamali Wanawake Watakiwa Kuzitimia Vizuri Fedha za Mikopo

Na.Mwandishi Wetu.

Wajasiriamali Wanawake Nchini wametakiwa kuzitumia vizuri fedha za Mikopo wanazozichukuwa kwa kuanzisha Biashara ndogondogo, zitakazo wasaidia kurejesha kwa wakati Mikopo hiyo.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya jamii, jinsi na Watoto Bi.Siti Abasi Ali wakati alipokuwa akizungumza na Wajasiriamali Wanawake katika Shehia ya Mgambo Wilaya ya Kaskazini ‘‘B’’.

 

Amesema idadi kubwa ya Wanawake wanachukuwa Mikopo lakini haifikii malengo kutokana na baadhi yao kuitumia bila ya malengo kwa kutumia katika Shughuli za Harusi, Chai na Wengine kuwapa Waume zao jambo ambalo linawapa ugumu wakati wa kurejesha Mkopo hiyo.

 

‘‘Baadhi ya Wanaume wakiona unataka kuchukuwa Mkopo wanakuwa na mapenzi ya hali ya juu lakini ukishapata Mkopo mukishanunulia Tasi na Mapembe wanakimbia na wiki nzima humuwaoni na kukuachia mzigo wa Deni peke yako.’’ alisema Mkurugenzi Siti.

 

Aidha amewashauri Wajasiriamali hao Wanawake kuangalia uwezekano wa kumiliki Ardhi ili iweze kuwasaidia wakati inapotokeza matatizo ikiwemo ya kutengana kwa familia.

 

Amefahamisha kuwa lengo la Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha anawanayanyua Wanawake Wajasiriamali kiuchumi kwa kupata Mikopo isiokuwa na Riba ili wajiendeshe na kuepukana na utegemezi.

 

Hata hivyo amesema Serikali inakusudia kujenga Vituo maalum vya Wajasiriamali Wanawake ili wapate sehemu za kukutana na kujadili masuala yao ikiwemo mbinu za kupata fursa zilizopo kupitia Mikopo ya Benki ya CRDB ambayo haina Riba.

 

Mbali na hayo amewakumbusha Wajasiriamali hao kushirikiana, kupendana na kuoneana huruma ili kuweza kufikia malengo ya Serikali kuhamasisha Wananchi kuanzisha Vikundi vya Ushirika katika maeneao yao.

 

‘‘Sio vizuri kusemana kwa wale wenzetu walioshindwa kutoa pesa katika vikundi na badala yake tuangalie mbinu mbadala ya kuweza kuwasaidia kulipa hivyo ninakuombeni Wanawake wenzangu tustahamiliane kwani aibu ya Mwanamke mwenzako ni yako’’. alisisitiza Mkurugenzi huyo.

 

Kwa upande wake Afisa maendeleo ya jamii, jinsia na Watoto Wilaya ya Kaskazini ‘‘B’’ Zuwena Hamad Omar amesema lengo la kufanya ziara hiyo ni kubaini changamoto walizonazo Wanawake Wajasiriamali katika Wilaya hiyo na kuzifikisha sehemu husika ili kutafutiwa Ufumbuzi wake.

 

Pia amewataka Mwenyeviti, Makatibu na Washika fedha wa Vikundi vya Ushirika katika Wilaya ya Kaskazini ‘‘B’’ kuwaunganisha pamoja Wanachama wao ili waweze kufikia malengo ya kuondokana na tatizo la Umasikini.

 

Mapema Wajasiriamali Wanawake katika Shehia ya Mgambo wamesema wanakabiliwa na matatizo mabalimbali ikiwemo Ukosefu wa fedha, Masoko, Vifungashio na Ofisi za kudumu kwa ajili ya kufanyia kazi kwani wanatumia Ofisi za kukodi jambo ambalo linapelekea kushindwa kufanya kazi kwa Ufanisi.

 

Hivyo wameiomba Serikali kupitia Wizara husika kujenga Vituo maalum vya Wajasiriamali Wanawake ili viweze kuwasaidia kukaa pamoja kujadili matatizo mbalimbali yanayowakabili katika vikundi vyao.

 

Jumla ya Vikundi 16 vya Wajasiriamali Wanawake na Wanachama zaidi ya 120 wameshiriki katika kikao hicho, kilichojadili masuala mbalimbali ya maendeleo katika vikundi vya Shehia ya Mgambo Wilaya ya Kaskazini ‘‘B’’.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.