Habari za Punde

Awamu ya Pili ya Mradi wa Maradhi Yasioambukizi Kuzinduliwa

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Maradhi Yasiyoambukiza (ZNCDs)  Dkt . Said Gharib Bilali (wa pili kulia)  akizindua mradi wa awamu ya pili  wa kukinga na kudhibiti  Maradhi yasiyoambukiza  kuwa  kipaumbele cha Afrika Mashariki katika Jumuiya ya Umoja wa Watu Wanaishi na Maradhi Yasioambukiza Zanzibar huko Mpendae Wilaya ya Mjini
Meneja wa Jumuiya ya Umoja wa Watu Wanaishi na Maradhi Yasioambukiza Zanzibar (ZNCDs) Haji Khamis Fundi (kushoto )akifahamisha kuhusu lengo la mradi huo kwa wanachama wa jumuiya hiyo  (hawapo pichani ) katika Jumuiya ya Umoja wa Watu Wanaishi na Maradhi Yasioambukiza Zanzibar huko Mpendae Wilaya ya Mjini .

Baadhi ya wanachama wa jumuiya hiyo  wakimsikiliza  

Meneja wa Jumuiya ya Umoja wa Watu Wanaishi na Maradhi Yasioambukiza Zanzibar (ZNCDs) Haji Khamis Fundi akitoa ufafanuzi juu ya mradi wa awamu ya pili wa kukinga na kudhibiti  Maradhi yasiyoambukiza  kuwa  kipaumbele cha Afrika Mashariki katika Jumuiya ya Umoja wa Watu Wanaishi na Maradhi Yasioambukiza Zanzibar huko Mpendae Wilaya ya Mjini .

 

Na Khadija Khamis – Maelezo .13/04/2024.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Maradhi Yasiyoambukiza (ZNCDs)  Dkt . Said Gharib Bilali  amesema Maradhi yasiyoambukiza yanahitaji kupewa kipaumbele Kwa kuzingatia utoaji wa elimu na huduma sahihi za afya ili kuweza kuzuwia Vifo vya mapema vinavyotokana na maradhi hayo.

 

Hayo yameelezwa wakati wa uzinduzi wa mradi wa Awamu ya pili  wa kukinga na kudhibiti  Maradhi yasiyoambukiza  kuwa  kipaumbele cha Afrika Mashariki katika Jumuiya ya Umoja wa Watu Wanaishi na Maradhi Yasioambukiza Zanzibar huko Mpendae Wilaya ya Mjini .

 

 Amesema ni vyema jamii kupatiwa elimu ya maradhi hayo ili kupata uwelewa wa kuweza kupambana nayo kutokana na vichocheo na athari zake.

 

Aidha ameeleza kupatiwa  taaluma ya maradhi hayo kutaisaidia jamii kujikinga na kujiwekea utaratibu wa  kuchunguza afya zao jambo ambalo litasaidia kupunguza  ongezeko la wagonjwa hao.

Amesema kuendelea kuzidisha juhudi za utoaji wa elimu na huduma Bora za kiafya kutasaidia kupambana na Maradhi hayo .

 

 

Amefahamisha kuwa mashirikiano ya pamoja kwa wadau mbali mbali  pamoja na Serikali kutaongeza juhudi ya kupambana na changamoto ya maradhi yasioambukiza .

 

Nae Meneja wa Jumuiya ya Umoja wa Watu Wanaishi na Maradhi Yasioambukiza Zanzibar (ZNCDs) Haji Khamis Fundi amesema lengo la mradi huo ni kuihamasisha jamii kufuata maelekezo ya wataalamu ili kupunguza vifo vya mapema vinavyotokana na maradhi hayo .

 

“Jamii ikipewa uelewa wa kutumia mfumo bora wa ulaji kufanya mazoezi kuacha kutumia vilevi sigara na tumbaku , kupima afya kutasaidia kupunguza ongezeko la vifo ” amefahamisha Meneja huyo .

 

Kwa upande wa wanachama wa jumuiya hiyo wakielezea changamoto mbali mbali wanazokumbana nazo ikiwemo kukosa huduma za NCD katika vituo vyao vya karibu pamoja na uhaba wa watoaji huduma za maradhi hayo .

 

Jumuiya ya maradhi yasioambukiza ni mkusanyiko wa Jumuiya za nchi mbali mbali za Afrika Mashariki ikiwemo Burundi,  Kenye,  Ruwanda, Tanzania, Uganda na Zanzibar zenye lengo la kupunguza vifo vya maradhi ya NCDs katika nchi zao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.