Habari za Punde

DKT. NCHEMBA AIOMBA INDONESIA KUSHIRIKIANA NA TANZANIA KUBORESHA MIFUMO YA KODI

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kulia) akieleza umuhimu wa ushirikiano katika maendeleo wakati wa mkutano na Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Mhe. Tri Yogo Jatmiko (hayupo pichani) katika Ukumbi wa Waziri wa Fedha Treasury Square, jijini Dodoma.  

Na. Benny Mwaipaja, Dodoma.

WAZIRI wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameiomba Indonesia kushirikiana na Tanzania kuboresha mifumo ya kodi ili kuboresha ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kuondoa changamoto zinazowakabili walipakodi nchini.

Dkt. Nchemba ametoa ombi hilo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Mhe. Tri Yogo Jatmiko, Jijini Dodoma ambapo walijadiliana mambo muhimu ya kuimarisha ushiriakiano kwa manufaa ya nchi hizo mbili.

Alisema kuwa Tanzania inakabiliwa na changamoto ya idadi ndogo ya walipa kodi pamoja na kuwepo kwa idadi kubwa ya wafanyabiashara walioko katika sekta isiyo rasmi hivyo mfumo thabiti wa kodi unahitajika ili kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na kuongeza idadi ya walipakodi.

Dkt. Nchemba alisema kuwa Indonesia ni miongoni mwa nchi zilizopiga hatua kubwa ya mifumo ya kodi na kwamba Tanzania itanufaika na ujuzi huo kwa kuwapa ujuzi zaidi maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania na Wizara ya Fedha kwa ujumla kujifunza Indonesia ilivyofanikiwa katika eneo hilo.

Aidha, Dkt. Nchemba aliishukuru Indonesia kwa mchango wake katika maendeleo ya nchi ambapo nchi hiyo imesaidia miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii pamoja na kutoa ujuzi na utaalam kwa watanzania katika nyanja mbalimbali.

Katika mazungumzo yao, Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Mhe. Tri Yogo Jatmiko, aliahidi kuwa nchi yake iko tayari kuendelea kuwapa ujuzi watanzania katika masuala mbalimbali ikiwemo sekta za nishati, kilimo na biashara na kwamba iko tayari pia kuwajengea uwezo watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA namna ya kujenga na kutumia mifumo ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato.

Aidha aliahidi kuwa ataendelea kuhamasisha wafanyabishara kuja kuwekeza nchini ambapo amesema idadi kubwa ya wawekezaji kutoka nchini Indonesia wamekuwa wakiulizia mara kwa mara kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo nchini, yakiwemo masuala ya utalii.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati) akiwa na ujumbe kutoka Wizara ya Fedha wakati wa mkutano kati yake na Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Mhe. Tri Yogo Jatmiko (hayupo pichani), ulioangazia ushirikiano kati ya Tanzania na Indonesia, uliofanyika katika Ukumbi wa Waziri wa Fedha Treasury Square, jijini Dodoma.
Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Mhe. Tri Yogo Jatmiko (katikati) akiwa na ujumbe kutoka ubalozi huo wakati wa mkutano kati yake na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hayupo pichani), ulioangazia ushirikiano kati ya Tanzania na Indonesia, uliofanyika katika Ukumbi wa Waziri wa Fedha Treasury Square, jijini Dodoma. 
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati) na Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Mhe. Tri Yogo Jatmiko (wa nne kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka Ubalozi wa Indonesia na Wizara ya Fedha baada ya kumalizika kwa mkutano ulioangazia ushirikiano kati ya Tanzania na Indonesia uliofanyika katika Ukumbi wa Waziri wa Fedha Treasury Square, jijini Dodoma. 
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kulia) na Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Mhe. Tri Yogo Jatmiko, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukutana na kufanya mazungumzo kuhusu ushirikiano kati ya Indonesia na Serikali katika kuchangia maendeleo, katika Ukumbi wa Waziri wa Fedha Treasury Square, jijini Dodoma.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Dodoma)


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.