SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesema imepiga hatua kubwa kwenye kukidhi ukuaji wa sekta ya usafiri wa anga kwa kufanikisha miradi kadhaa ya sekta hiyo kwa nia ya kuongeza ufanisi na kukuza utalii wa nchi kwa maendeleo ya Taifa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo alipofungua Kongamano la Sita la Usafiri wa Anga la Jumuiya ya Afrika Mashariki, hoteli ya Verde, Mtoni
Mkoa wa Mjini Magharibi.
Alisema, Sekta ya Utalii ni muhimu kwa mikakati ya maendeleo ya uchumi
wa nchi na Usafiri wa Anga ni kichocheo kikuu cha ukuaji wa Uchumi hasa kwenye kufikia
malengo ya nchi iliyojiwekea kupitia sekta ya utalii na biashara kuna haja ya kusaidia
ipasavyo sekta ya usafiri wa anga.
Akizungumzia
mafaniko ya sekta ya usafiri wa Anga kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
Rais Dk. Mwinyi alisema, Serikali imekamilisha mradi wa ujenzi wa jengo jipya
la abiria (Terminal 3) kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani
Karume ambalo kwasasa linafanyakazi kwa ufanisi mkubwa wa kutoa huduma za
usafiri wa anga Zanzibar.
Pia alieleza,
Serikali imeanza ujenzi wa jengo jipya la abiria (Terminal 2) lenye ukubwa wa
mita za mraba 16,000 litakuwa na uwezo wa kuhudumia zaidi ya abiria 1,300,000
kwa mwaka ambalo awali lilijengwa mwaka 1974 kwa sasa linahitaji marekebisho
makubwa pamoja na ujenzi wa sehemu ya kuegesha magari yenye uwezo wa kuhudumia
magari zaidi ya 200 kwa wakati mmoja.
Dk. Mwinyi pia alisema, Serikali inatekeleza mradi
wa ujenzi, ukarabati na uboreshaji wa jengo la zamani la (Terminal 1) kwenye Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume ambalo awali lilijengwa miaka ya
1950 pamoja na kutekeleza mradi wa ujenzi wa Kituo cha biashara, kitakachojumuisha maduka, migahawa, huduma za
kibenki na ofisi, ujenzi wa eneo la kuhifadhi na kusafirisha chakula pamoja na ujenzi wa vituo vipya vya
kutolea huduma za mafuta ya anga kwa makampuni ya Oilcom, GBP na Lake Oil.
Alieleza,
Serikali pia inatekeleza mradi wa ujenzi na utanuzi wa Uwanja wa ndege wa Pemba unaojumuisha
upanuzi wa urefu wa njia ya kurukia ndege kutoka mita 1,525 hadi mita 2,510,
ujenzi wa maegesho ya ndege (apron) yenye uwezo wa kuchukua ndege mbili kubwa
aina ya Code C (B 737-800) na ndege 8 ndogo za Code B na ujenzi wa jengo jipya
la abiria lenye ukubwa wa mita za mraba 9,170 pamoja na ujenzi wa Uwanja cha ndege
wa Nungwi unaolenga kuhudumia zaidi shughuli za utalii zinazoongezeka Zanzibar.
Dk. Mwinyi alieleza,
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inazingatia mikataba yote ya usafiri wa anga ya
kimataifa ili kuhakikisha ukuaji wa sekta hiyo unaendelea kuwa salama.
Pia alieleza, Tanzania
inajivunia mafanikio yaliyofikiwa kwenye sekta ya usafiri wa anga kwa kuendelea
kushirikiana na nchi washirika chini ya mwavuli wa Taasisi ya Udhibiti wa
Usalama wa Usafiri wa Anga ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, katika kuoanisha
kanuni za usafiri wa anga ndani ya ukanda huo kwa lengo la kuoanisha taratibu,
kuimarisha usalama, na kuongeza ufanisi.
Alisema, Serikali imeboresha mradi wa Masafa ya Mbali (VHF)
unaojumuisha ufungaji wa vituo 18 vipya na redio kwenye Viwanja vya Ndege 12,
na uwekaji wa mifumo ya kinasa sauti katika viwanja vinne vya ndege, Uwekaji wa
Mfumo wa Kutua kwa ndege (ILS) kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid
Aman Karume.
Aidha, Dk. Mwinyi alieleza
mwaka jana Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipata asilimia 87 katika
kuhakikisha usalama na ufanisi kwenye Mpango wa Kimataifa wa Ukaguzi wa Usalama
wa Kimataifa, uliofanywa na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO) ukiwa
na lengo la kukuza usalama wa usafiri wa anga duniani kupitia ukaguzi na
ufuatiliaji wa mara kwa mara wa utendaji wa usalama wa anga wa Nchi Wanachama.
Hivyo, aliwata wadau na
washirika wa usafiri wa anga kuimarisha ushirikiano ili kuhakikisha sekta hiyo
inaendelea kukua kwa usalama sambamba na kuwa himiza kujadili na kutoa
mapendekezo sio tu jinsi changamoto zilizoainishwa katika maeneo hayo
zinavyoweza kutatuliwa, bali pia kubainisha jinsi fursa zinazohusiana na maeneo
hayo zinavyoweza kutumika kikamilifu kwa manufaa ya usalama wa anga, uwezo,
ufanisi na ulinzi wa mazingira kwenye Ukanda wa nchi za Afrika Mashariki.
Naye, Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi, Dk. Khalid Muhamed Salum
alisema Sekta ya usafirishaji wa Anga inakisia zaidi ya abiria milioni tatu
husafiri kwa anga kila siku kutokana na umuhimu wa haraka wa safari zake.
Hivyo aliwasiri washiriki wa kongamano hilo wakiwemo nchi wanachama
kujadili kwa kina masuala ya usalama, gharama na ufanisi ili kuwe kupatikane
tija kwa changamoto zilizomo kwenye sekta hiyo.
Sambamba na kuahidi Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoa ushirikiano
kwa wadau hao ikiwemo Serikali ya Jamuhiri ya Muungano wa Tanzania.
Kongamano
la Sita la Usafiri wa Anga la
Jumuiya ya Afrika Mashariki, umewakutanisha wadau wa tasnia hiyo kwa siku mbili
mfululizo ukiwa na kauli mbiu “Mustakabali wa
Usafiri wa Anga: Kudumisha Mifumo ya Usafiri wa Anga yenye Ustahimilivu,
Uendelevu, Ubunifu na Usalama" limezishirikisha nchi wanachama kutoka mataifa ya
Afika Kusini, Burundi, Jamuhuri ya Demokrasia ya Congo, Kenya, Ethiopia,
Somalia, Sudani Kusini, Rwanda na mwenyeji Tanzania ikiwemo Zanzibar. Mwezi
Febuari mwaka 2020 kongamano kama hilo lilifanyika jijini Bujumbura, Burundi.
IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment