Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni amewataka Askari na Maafisa wa Vyombo vya Usalama vilivyopo chini ya wizara hiyo kutenda kazi kwa kufuata haki na uadilifu katika kuwahudumia wananchi baada ya Askari na Maafisa hao kupandishwa vyeo na Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan hivi karibuni.
Ameyasema hayo,leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua Kikao cha Tume ya Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto na Uokoaji na Uhamiaji ambapo kwanza amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa upandishaji huo ambao ulikoma takribani kwa miaka mitano.
‘Ni Imani yangu sasa kwamba mashauri yote yaliyokuwa hayajashughulikiwa sasa tume itaweza kuyashughulikia lakini sasa niungane na Mkurugenzi wa Tume hii kumshukuru sana Amiri Jeshi Mkuu,Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa upandishaji vyeo ambao aujaacha askari hata mmoja kuanzia ngazi ya chini mpaka juu sasa nendeni mkavitendee haki vyeo hivyo,haki uenda na wajibu naombeni mkawe waadilifu na mkafanye kazi alizokusudia Mheshimiwa Rais ya kuzuia na kupambana na uhalifu,huko chini vilio ni vingi nendeni mkavisikilize na mvitafutie ufumbuzi’.alisema Waziri Masauni
Akizungumzia moja ya changamoto alizokumbana nazo wakati akifanya ziara katika vyombo,Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Daniel Sillo aligusia hoja iliyoibuliwa na askari mbalimbali wa Jeshi la Magereza waliokua wakiulizia zoezi la upandishaji vyeo ambalo ulipita muda mrefu bila kupandishwa vyeo na sasa anashukuru kuona hoja hiyo imefanyiwa kazi.
Akizungumzia zoezi hilo la Upandishwaji vyeo Mkurugenzi Msaidizi wa tume hiyo,Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi,George Mwansasu alitaja idadi ya waliopandishwa vyeo,Jeshi la Polisi Maafisa Wandamizi waliopandishwa ni 154,Zimamoto na Uokoaji Maafisa Wandamizi 11,Jeshi la Uhamiaji waliopandishwa ni Maafisa Waandamizi 50 na Jeshi la Magereza waliopandishwa ni 50.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu wa wizara hiyo,Miriam Mmbaga akiweka wazi juu ya kuongezeka kwa ufanisi wa utendaji kazi baada ya kuongezeka kwa rasilimaliwatu ambayo katika vyombo vya usalama upandishwaji vyeo huo unaendana na utoaji na usimamizi wa majukumu katika shughuli zao za kila siku.
No comments:
Post a Comment