Habari za Punde

UNICEF Yaimwagia Sifa Tanzania kwa Uwazi katika Maandalizi na Utekelezaji wa Bajeti

Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Bi. Elke Wisch, wakionesha moja ya chapisho la shirika hilo kuhusu Utafiti wa Utekelezaji wa Bajeti (Budget Survey), baada ya kikao chao kilichofanyika jijini Dodoma, ambapo wamejadiliana masuala mbalimbali ya maendeleo na ushirikiano na pia shirika hilo limeipongeza namna Tanzania inavyofanya vizuri katika masuala ya bajeti.
Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) ukiwa katika kikao na ujumbe kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF), ulioongozwa na Mwakilishi Mkazi wa Shirika hilo nchini, Bi. Elke Wisch, ambapo wamejadiliana masuala mbalimbali ya maendeleo na ushirikiano, ikiwemo namna Tanzania inavyofanya vizuri katika masuala ya bajeti.

Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati), na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF), Bi. Elke Wisch (wa saba kushoto), wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe kutoka Shirika hilo na ujumbe kutoka Wizara ya Fedha, baada ya kikao chao jijini Dodoma, ambapo wamejadiliana masuala mbalimbali ya maendeleo na ushirikiano ikiwemo namna ambavyo Tanzania inavyofanya vizuri katika masuala ya bajeti.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma)


Na Benny Mwaipaja, WF, Dodoma

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), limeipongeza Tanzania kwa kupiga hatua kubwa katika masuala ya uwazi kwenye mchakato wa uandaaji na utekelezaji wa Bajeti Kuu ya Serikali kutokana na matokeo ya utafiti wa uliofanywa na Shirika hilo.

Pongezi hizo zimetolewa jijini Dodoma na Mwakilishi Mkazi wa UNICEF nchini Tanzania, Bi. Elke Wisch, alipokutana na kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) ambapo walijadiliana mambo mbalimbali ya ushirikiano kati ya Serikali na UNICEF.

Kutokana na utafiti walioufanywa na UNICEF, utakaozinduliwa hivi karibuni unaonesha kuwa katika kipindi cha miezi 16 iliyopita ambacho utafiti huo umefanyika, Tanzania imepanda viwango vya uwazi katika masuala ya bajeti kutoka asilimia 21 hadi 41 na kuzizidi nchi zote za Bara la Afrika.

Alisema kuwa katika kipindi cha Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tanzania imepiga hatua kubwa katika suala la uwazi na uwajibikaji kutokana na bajeti yake kuwa na uhalisia na kuweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara, wawekezaji, wadau wa maendeleo na taasisi za fedha.

Bi. Wisch alisema kuwa hatua hiyo inafaa kupongezwa na wadau wote wa maendeleo na kwamba matarajio ya Shirika hilo ni kuona kiwango hicho kinaongezeka zaidi ili angalau kifikie zaidi ya asilimia 50, jambo ambalo alisema kutokana na uongozi thabiti wa Serikali ya Awamu ya Sita, viwango hivyo vitafikiwa hivi karibuni.

Bi. Wisch ameahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika masuala mbalimbali ya maendeleo hususani masuala ya elimu, lishe, Watoto na vijana.

Aidha, Bi. Wisch alieleza kuwa Tanzania ina programu za chakula mashuleni jambo ambalo linawasaidia wanafunzi kuwa na mazingira mazuri ya kupata elimu, lakini pia msisitizo wa lishe bora kwa Watoto ni jambo muhimu ili kupambana na udumavu wa akili na kuwajengea watoto ubongo unaomuwezesha mtoto kuwa na akili nzuri.

Alisema pia kuwa Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika masuala mbalimbali ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika jambo ambalo linachochea ushirikiano zaidi na mashirika ya maendeleo katika kusaidia kuchochea zaidi maendeleo ya wananchi wake katika sekta mbalimbali.

Kwa upande wake Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba alisema kuwa katika Bajeti Kuu ya mwaka wa fedha 2023/24 UNICEF, iliahidi kutoa msaada wa zaidi ya dola milioni 20.3 kwa ajili utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya uchumi wa kijamii kwenye  eneo la afya, lishe, elimu, kuwalinda Watoto, sera ya jamii, jinsia na mipango.

Dkt. Nchemba ameipongeza UNICEF kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali zinazokuza ustawi wa jamii kupitia michango yao katika Bajeti Kuu ya Serikali zinazoelekezwa kuhudumia jamii ikiwemo afya na elimu.

Aidha Dkt. Nchemba amelishukuru Shirika hilo kwa msaada wake katika masuala ya uwazi, uwajibikaji na kusaidia ushiriki wa umma katika hatua mbalimbali za maandalizi ya bajeti kupitia utafiti wao wa uwazi wa masuala ya bajeti.

Alisema kuwa Tafiti hizo zimesaidia kuboresha bajeti jambo lililosaidia kujenga imani ya wananchi kwa Serikali yao na matumizi bora ya rasilimali.

Amesema kuwa anatumaini  UNICEF itaendelea kuisaidia Serikali katika masuala ya kibajeti na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano ulioanzia mwaka 2021/22 hadi 2025/26.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.