Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Amefanya Ziara Kutembelea Mradi wa Ujenzi wa Skuli Nne Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akitoa maagizo kwa Mshauri elekezi kutoka Wakala wa Majenzi (ZBA) kusimamia vyema Ujenzi wa Mradi wa Skuli ya Sekondari ya ghorofa iliopo Chukwani Wilaya ya Magharibi "B" Unguja wakati wa ziara yake ya kukagua Maendeleo ya Ujenzi wa Mradi huo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameitaka Kampuni ya Fuchs Contraction Ltd ambayo imepewa dhamana ya kujenga skuli nane (8) za Gorofa kuhakikisha wanakamilisha ujenzi huo ndani ya muda uliopangwa na kiwango kilichokusudiwa ili kutoa nafasi kwa wanafunzi kusoma katika mazingira mazuri.

Ameyasema hayo katika ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa skuli zinazojengwa na Kampuni hiyo ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kutembelea Miradi ya Maendeleo.

Mhe. Hemed amemuagiza Mkandarasi wa majengo hayo  kuongeza nguvu kazi na kufanya kazi mchana na usiku ili kuhakikisha Miradi hio inakamilika kwa wakati na kiwango kilichokusudiwa ili kuwaondolea changamoto wanafunzi ya kufata elimu masafa ya mbali jambo ambalo linapunguza umakini na ufaulu kwa wanafunzi hao.

Amesema mtazamo na adhma ya Rais Dkt Hussen Mwinyi ni kujenga skuli za kisasa zenye viwango na zenye kuendana na wakati sambamba na kuweka vifaa vya kutosha vya kufundishiia ili  kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani pamoja na kuingia mkondo moja tu kwa wanafunzi wote wa Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa kila aina ya ushirikiano kwa wakandarasi hao na  kuwahakikishia kuwa kiwango cha fedha kilichobakia kitalipwa ndani ya siku chache zijazo ili kuharakisha umalizikaji wa ujenzi huo na wanafunzi waliopangishwa katika maskuli jirani waweze kurejea maskuli mwao.

Nae Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Ali Abdulghulam Hussein amesema ziara ya kutembelea Miradi ya Ujenzi wa Skuli za gorofa zinazoendelea kujengwa itatoa matokeo chanya ndani ya muda mfupi ujao na uongozi wa wizara utahakikisha majengo yote yanamalizika kwa kiwango cha hali ya juu.

Naibu Waziri Ghulam amesema vifaa vyote kwa ajili ya maskuli yanayojengwa Zanzibar vipo tayari na Wizara imetenga Bajeti kwa ajili ya kuyafanyia ukarabati mkubwa maskuli yote yaliyoanza kuchakaa ili yaendane na hadhi ya majengo yanayojengwa sasa.

Kwa upande wake Mwakalishi wa mmiliki wa Kampuni ya Fuchs Contraction Ltd Ndugu YASIN FEISAL IBRAHIM amesema Kampuni imejipanga kufanya kazi usiku na mchana na kuahidi kukamilisha ujenzi wa maskuli hayo kwa ubora na viwango vya hali ya juu ifikapo mwishoni mwa mwezi wa nane(8).

Mkandarasi Feisal amesema kulikuwa na changamoto ndogo ndogo ambazo zilikwamisha ujenzi huo lakini kwa sasa kila kitu kipo sawa hivyo watahakikisha wanapambana ili waweze kukabidhi kwa wakati na kutumia fursa hio kuiomba Serikali kuwamalizia malipo ya fedha zilozobaki ili kazi iendelee kwa haraka zaidi.

Mapema Mshauri elekezi kutoka wakala wa majengo Zanzibar (ZBA) MOH'D NAHODA MOH'D amesema makubaliano ya awali na Kampuni ya Fuchs ni kukamilisha Ujenzi huo mwishoni mwa mwezi wa saba(7) lakini imekuwa tofauti na ujenzi huo unaonekana kusuasua jambo ambalo linachelewesha mipango ya Serikali ya kuboresha miundombinu ya Sekta ya Elimu kama ilani ya Chama cha Mapinduzi inavyoelekeza.

Mkandarasi Nahoda amesema endapo kampuni ya Fuchs itashindwa kukamilisha kwa wakati miradi hio ZBA kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali watangali ni kwa namna gani wanaweza kufanya maamuzi ya kisheria dhidi ya kampuni hio ili kuwaweka sawa wakandarasi wengine waliopewa dhamana ya kujenga miradi ya Serikali.

Katika ziara hio makamu wa pili wa rais wa Zanzibar ametembelea ujenzi wa skuli za ghorofa ikiwemo CHUMBUNI, MAUNGANI, MWERA, REGEZAMWENDO, KIJICHI, CHUMBUNI na MUUNGANO.

Imetolewa na Kitengo Cha Habari (OMPR)

Leo tarehe 02.07.2024.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.