Habari za Punde

Bima ya msafiri kuanza rasmi kesho 1 Oktoba


 NA FAUZIA MUSAA

WAZIRI wa Utalii na mambo ya kale, Mudrik Ramadhan Soraga amewashauri wageni wanatarajia kuingia nchini kufanya maombi ya   bima ya msafiri  kwa njia ya mtandao  wakiwa nchini kwao ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo mara tu wanapowasili Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukamilika kwa zoezi la mfano wa utekelezaji wa bima ya msafiri katika viwanja vya ndege vya Kimataifa  vya Zanzibar (AAKIA) inayotarajiwa kuanza rasmi  Oktoba mosi 2024, alisema hatua hiyo itawasaidia  wageni kuondokana na changamoto zinazoweza kujitokeza endapo wataanza kufanya zoezi hilo baada ya kuingia Nchini.

Alifahamisha kuwa kutokana na kuwa huduma hiyo ni mpya changamoto ndogondogo zinaweza kujitokeza na kuzitaka Taasisi na mamlaka  husika kuzifanyia kazi kwa haraka changamoto hizo endapo zitajitokeza  ili kuenda sambamba  na viwango vya Kimataifa vya  utoaji wa huduma hiyo.

Alisema matarajio ya Wizara ya Utalii ni kuona wageni hao hawakwaziki kupitia huduma hiyo na kuwataka kuwahudumia kwa haraka bila kuathiri harakati zao.

" Mgeni mmoja atumie dakika  zisizozidi kumi kukamilisha hatua zote za kupata huduma hiyo, ili kuwapa muda wa kuendelea na shughuli zao, haiwezekani mtu katumia masaa 8 kwa ajili ya safari halafu atumie tena masaa 3 uwanja wa ndege kupata huduma hii." Alisema Soraga

Hata hivyo alizisisitiza Mamlaka na Taasisi hizo kuendelea kutoa elimu kwa wageni juu ya utaratibu na umuhimu wa kupata huduma hiyo iliyoanzaishwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Naye Meneja wa Bima Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC), Sabri Omar Ali,  alisema wameandaa zoezi hilo la mfano ili kuona watakavyomudu kutoa huduma kwa makundi ya  wageni wanaoingia nchini bila kuanza taratibu za kupata huduma hiyo  tangu wanapotokea.

Alieleza kuwa abiria 300 wa mfano walishiriki zoezi hilo  kwa lengo la kuona mapungufu na  changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji  na kuzifanyia kazi ili kuimarisha huduma hiyo.

“katika zoezi hili la mfano tumebaini baadhi ya changamoto ndogondogo ambazo tunazichukua kwenda kuzifanyia kazi ili  kuboresha utoaji wa huduma hii pale itakapoanza rasmi utekelezaji wake.” Alifahamisha meneja Sabri

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeanzisha bima ya msafiri kwa lengo kuwasaidia wageni wanapopata hitilafu za kiafya na kutumika kwa majanga yote watakayopata wageni hao wakiwa nchini au katika mipaka ya Tanzania.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.