RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Mapinduzi makubwa katika sekta ya
Miundombinu ya Bandari yanalenga kuifanya Zanzibar kuwa kituo muhimu cha
Usafirishaji na kupokea Meli kubwa zinazoleta bidhaa nchini.
Rais Dk. Mwinyi ametoa tamko hilo leo tarehe 18 Oktoba
alipoifungua Bandari kavu ya Maruhubi, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amefahamisha kuwa ufunguzi wa Bandari kavu ni hatua muhimu ya
kuimarisha utendaji wa bandari kwani itapunguza msongamano wa makontena katika
Bandari ya Malindi.
Rais Dk. Mwinyi ameeleza, mabadiliko hayo ya Miundombinu ya
Bandari yataleta msukumo mkubwa wa ukuaji wa Uchumi wa Zanzibar na kuwasisitiza
wadau kuunga mkono juhudi hizo.
Ameeleza kuwa kampuni ya Africa Global
Logistic inayoendesha bandari ya Malindi hivi sasa inaendelea kuleta
mabadiliko makubwa ya kiutendaji yanayoongeza Ufanisi na kuwapa urahisi
Wafanyabiashara kutekeleza wajibu wao bila usumbufu pamoja na kuokoa muda.
Dk. Mwinyi amewahakikishia wadau kuwa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, itaendelea kufanya kazi zaidi na sekta binafsi kwani mbali ya kuja na
mitaji, pia wanakuja na utaalamu na teknolojia za kisiasa zinazochochea ufanisi
kwenye utendaji.
Rais Dk. Mwinyi amesisitiza kuwa Serikali ianendelea na Ujenzi
wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani kwa kuifanya kuwa yenye uwezo wa
kuhudumia meli nyingi zaidi ikwemo kampuni za kimataifa kuleta meli za mafuta kwenye
bandari hiyo.
Amesisitiza, bado kuna fursa zaidi za kuongeza kasi ya utoaji wa
huduma kwa bandari zote na kuziagiza taasisi za TRA, ZBS, ZFDA, taasisi ya
Atomic energy, na Mkemia Mkuu wa Serikali kuongeza kasi na ufanisi katika
utendaji wao ili kuwarahisishia Wafanyabiashara mazingira bora ya ufanyaji wa
biashara yatakayopunguza gharama na kumpa unafuu mtumiaji.
Amebainisha kuwa Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi
imedhamiria kuendesha huduma za bandari kwa ufanisi zaidi kwa kuzingatia
bandari ni lango kuu la uchumi kwa nchi.
Aidha, amesema Serikali
kupitia mradi huo utawapunguzia gharama kubwa wafanyabiashara.
Ameeleza hatua hiyo pia itasaidia harakati za
uendeshaji kuwa zenye ufanisi, kuongeza tija na kupunguza gharama za uletaji
mizigo (freight price) ndani ya nchi.
Pia Rais Dk.
Mwinyi amewahakikishia wafanyabiasha kuwa Serikali inaendelea kuwawekea mazingira rafiki hasa kwa
ujenzi wa miundombinu.
Alisema, Serikali inashirikiana na
wadau mbalimbali ili kuendeleza sekta ya Uchukuzi na kuimarisha jitihada za
pamoja za kuleta mafanikio ya kuimarisha miundombinu ya barabara, bandari na viwanja
vya ndege Unguja na Pemba ili kuwarahisishia huduma wananchi na wageni wanaoitembelea
Zanzibar.
Aidha, Dk. Mwinyi amesihi
wafanyabiashara kuendesha shughuli zao kwa kuwazingatia wananchi hasa kuwapunguzia
makali ya bei za bidhaa kutokana na hatua zinazochukuliwa na Serikali za kupunguza
gharama za usafiri.
Waziri
wa Mawasiliano, Usafirishaji na Uchukuzi Dk. Khalid Salum Muhammed amesema,
mageuzi na mafanikio yaliyofikiwa kuimarisha sekta ya Bandari ni
utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2020 – 2025.
Aidha,
amesisitiza kuwa mabadiliko yanayoendelea kwa kuziimarisha Bandari yanaenda
kuifanya Zanzibar kufikia malengo na matarajio ya kuhudumia Meli takriban laki
tatu kwa mwaka.
Naye,
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari, Atif Khamis ameeleza dhana ya ushirikiano
baina ya Serikali na Sekta binafsi imekuwa kuchochea mabadiliko makubwa ya
utendaji wa shirika la Bandari na kuelezea ufunguzi wa Bandari kavu utaongeza maputo
ya Shirika na kupunguza msongamano wa Makontena bandari ya Malindi.
Amefahamisha,
ongezeko la mapato kwa asilimia 15 tangu kampuni binafsi kuingia ushirikiano na
Serikali kuiendesha Bandari ya Malindi, kupungua kwa muda wa Meli kusubiri
gati kwa asilimia 75 na muda wa kutoa Makontena kutoka siku 40 hadi siku 7 hadi
kumi hivi sasa kwa asilimia 50.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment