RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameitaja Sekta ya
Kilimo kuwa eneo muhimu litakaloimarisha ushirikiano wa dipolomasia baina ya
Tanzania na Iran.
Dk. Mwinyi amehimiza Ushirikiano huo
kwa kuisifu Iran kuwa ni wabozi kwenye teknolojia ya kilimo.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo Ikulu,
Zanzibar alipozungumza na Waziri wa Kilimo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Dr.
Gholamreza Nouri aliefika na ujumbe wa wataalamu 15 kutoka sekta mbalimbali za
maendeleo za nchi hiyo.
Dk. Mwinyi amesema Kilimo ni sekta
kubwa ya Uchumi wa Tanzania Bara kulingana na kubarikiwa kuwa na eneo kubwa
kijiografia, hivyo, ameisihi Iran kuimarisha ushirikiano kwa kubadilishana
uzoefu, mbinu na teknolojia kwenye eneo hilo.
Kuhusu Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi
amesema inajikita zaidi kwenye kilimo cha viungo (Spices) kutokana na sehemu kubwa ya uchumi wake
kutegemea soko la Utalii ambao unachangia asilimia kubwa ya uchumi wa nchi.
Pia, Dk. Mwinyi alimweleza mgeni wake
huyo kuhusu kuzihuisha na kuziimarisha sehemu za historia katika kukuza soko la
Utalii wa Urithi na kuboresha ushirikiano uliopo baina ya Tanzania hasa
Zanzibar na Iran kwenye eneo hilo la utalii.
Halikadhalika, Rais Dk. Mwinyi amegusia Sekta
ya Usafirishaji wa baharini na kuiomba Irani kuongeza ushirikiano kwenye eneo
hilo ili kuimarisha biashara na uchumi kupitia bandari za pande mbili hizo za
ushirikiano.
Akizungumzia ushirikiano na sekta binafsi
baina ya Tanzania kususan Zanzibar na Iran, Rais Dk. Mwinyi amamuahidi Waziri
huyo kwamba “Chamber of Commerce” ya Zanzibar itaimarisha ushirikiano na ya
Iran kuona Uchumi endelevu baina ya pande mbili hizo.
Naye, Waziri Dr.
Gholamreza alisifu
ushirikiano mzuri wa Diplomasia uliopo baina ya Iran na Tanzania na kuongeza kuwa
katika kuboresha ushirikino wao wameikaribisha Tanzania nchini kwao na
kuwaahidi kuwapa eneo la kufungua ubalozi wa Tanzania nchini Iran.
Pia Waziri huyo, amesema watasaini makubaliano
na Tanzania hasa Zanzibar kwenye sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo Kilimo, Utalii,
Elimu, Biashara na Sekta ya uhandisi pamoja na kuahidi kutoa ushirikiano na
kubadilishana uzoefu, mbinu na teknolojia kwenye maeneo hayo.
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment