Na.OMWKR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amewataka wataalamu wa Rasilimali watu na
Utawala kuhakikisha kwamba haki za watumishi katika sehemu za kazi zinalindwa sambamba
na kuthamaniwa utu wao.
Mhe. Makamu ameyasema hayo
alipomuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Husein Ali Mwinyi katika maadhimisho ya siku ya Rasilimali watu duniani yaliyofanyika katika hoteli ya New Aman
wilaya ya mjini Mkoa wa Mjini Magharib Unguja.
Mhe. Othman amewataka wataalamu hao
kuhakikisha kwamba wanasimamia vyema maadili , weledi na uadilifu , usawa na
ushirikishwaji hasa kwa watu wa makundi
maalumu katika sehemu za kazi.
Aidha amehimiza kuwepo mipango
maalum na endelevu ya kuwajengea uwezo watumishi kwa kutoa mafunzo mbali mbali
yenye lengo la kuongeza ufanisi na kuleta tija katika sehemu za kazi na taifa
kwa jumla.
Mhe. Othman ameeleza kwamba hatua
hiyo inatokana na ukweli kwamba hivi sasa taaluma ya rasilimali watu imegeuka
kuwa chombo muhimu cha kuleta mabadiliko ya kiutendaji na kwamba taaluma hiyo
kwa sasa inazidi kuwa ni mkakati wa msingi katika kuzidisha ufanisi kwenye
taasisi mbali mbali za kazi.
Hivyo, Mhe. Othman amesisititiza kwamba
kutokana na hali hiyo taifa linawajibu wa kuendeleza, kulinda na kuenua taaluma
hiyo ili izidi kutoa mchango katika
jitihada za taifa za kufanikisha kuleta maendeleo ya nchi.
Amesema kwamba kwa upande wa
serikali itaendelea kukuza mazingira bora kupitia uimarishaji na kufanya
mageuzi makubwa katika mifumo ya utoaji huduma na kiutumishi wa umma kwa kuimarisha uwazi na uwajibikaji
pamoja na kuhimiza matumizi ya TEHAMA katika usimamizi wa rasilimali watu na
kuleta maendeleo ya kiuchumi nchini.
Mhe. Othman amesema kwamba ni vyema juhudi hizo zikaungwa mkono kwa ushirikiano wa sekta zote kwa kuzingatia kwamba hivi sasa sekta binafasi nayo inaendelea kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa maendeleo ya kiuchumi.
Mhe. Othman amesisitiza kwamba
maendeleo ya taifa yatategemea sana ubora wa watu wake wenye ujuzi , maadili,
moyo wa kizalendo na uwezo mkubwa wa kutoa matokeo bora katika kazi mbali mbali
za kiutumishi wanazozifanya.
Amesema kutokana na hali hiyo,
serikali za Tanzania zinafanya juhudi kubwa katika uwekezaji wa rasilimali watu
kwa kuwapatia watumishi ujuzi na taaluma
za aina mbali mbali ili wawe chachu ya kufanikisha mipango mbali mbali ya
maendeleo ya taifa inayowekwa.
Aidha Mhe. Othman ametaka Taasisi
hiyo kuwasaidia watumishi na viongozi
mbali mbali wa Zanzibar kuwajenga kwenye utamaduni wa uwajibikaji bora na
kujenga nidhamu ya kazi na kuwafanya wafanyakazi watambue kwamba kazi
wanayofanya ni yao na sio ya muajiri .
Naye waziri wa Nchi Ofisi ya rais
Katiba, Sheria , Utumishi na Utawala bora
Haroun Ali Suleiman, amesema kwamba ni muhimu kwa taasisi na wadau mbali
mbali kukutana kujadili kuweza kuzipatia ufuimbuzi changamoto mbali ,mbali
zinazoikabili Jumuiya hiyo ya wanataaluma.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumiya ya Wanataaluma ya Raslimali watu Tanzania Christopher Kabalika Mwansasu, ameipongeza serikali kwa kuboresha maeneo ya huduma , kuimarisha mifumo ya rasilimali watu pamoja na kuwekeza kwenye nguvu kazi ya rasilimali watu ili kuliwezesha taifa kujiandaa na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yanayoendelea duniani.
Amesema kwamba Sekta ya rasilimali
watu ni muhimu katika kutoa mchango wa kukabiliana na mabadiliko yanayotokea
duniani na kuwa mshindani sahihi katika kusimamia kazi kwa viwango vya juu ili kuleta maendeleo kwani dhima ya wataalamu ni kusimamia
viango bora vya kazi na kufikia malengo ya kuwakilisha na kuendeleza ujuzi wa
wanachama katika majukwaa ya kitaifa na kimataifa ambako masuala ya rasilimali
watu yanajadiliwa.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha
wanataaluma ya Rasilimali watu Tanzania,
(THRAPA), Denes Dehua amesema kwamba
lengo kuu la taasisi hiyo ni kukuza
viwango vya taaluma kwa watumishi
pamoja na kulinda maadili katika
maendeleo ya rasilimali watu kwa kushirikiana na vyombo mbali mbali ikiwemo
serikali.
Mwisho
Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa
Kwanza wa Rais wa Zanzibar kupitia Kitengo chake cha Habari Leo Jumanne Mei 20,
2025.
No comments:
Post a Comment