Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla Amefunga Kongamano la Afya Zanzibar Lililofanyika katika Ukumbi wa Golden Tulip Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizindua kitabu cha Miongozo ya matibabu ya kawaida na orodha muhimu ya dawa kilichotolewa na Wizara ya Afya Zanzibar kwenye ufungaji wa Kongamano la wiki ya Afya Zanzibar lililofanyika katika Ukumbi wa Hotel ya Golden Tulip Zanzibar.

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe.Hemed Suleiman Abdulla, amesema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, itaendelea kuchukua jitihada zaidi za kuimarisha miundombinu na utoaji wa huduma za afya kwa wananchi, hatua inayolenga kuwa na jamii yenye siha bora.

Hemed ameyaeleza hayo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, alipomuwakilisha katika hafla ya ufungaji wa kongamano la wiki ya Afya Zanzibar.

Alisema katika uongozi wa awamu ya nane, serikali imejenga hospitali za kisasa kwa ngazi za wilaya na hospitali ya Mkoa ya Lumumba, ambayo inatoa huduma za kibingwa.

Amesema mbali ya ujenzi wa hospitali hizo za kisasa ambazo zimekuwa tegemo kubwa la utoaji huduma za matibabu kwa wilaya zote za Zanzibar, pia serikali imeziekea hospitali hizo vifaa tiba vya kisasa na upatikanaji wa dawa kwa uhakika.

Akitoa mfano, Makamu wa Pili wa Rais amesema serikali imeimarisha upatikanaji wa huduma
mbalimbali kama vile usafishaji wa figo, huduma za mama na mtoto, kuongeza wataalamu wenye sifa, kuimarisha maslahi ya wafanyakazi na kujenga nyumba za madaktari.

Alifahamisha kuwa pamoja na kazi kubwa iliyofanyika, serikali itaendelea kuiimarisha sekta hiyo ambapo mipango iliyopo ni kuhakikisha inasomesha madaktari ili wafikie ngazi za kibingwa na ubobevu, hatua ambayo itaongeza wigo wa utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Aidha, serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia wizara ya Afya iko kwenye mipango ya kujenga hospitali kubwa ya kisasa ya rufaa katika eneo la Binguni, ambapo hatua za awali za ujenzi wa hospitali hiyo zimeshakamilika

Mhe. Hemed ametoa wito kwa wataalamu wa sekta ya afya kuhakikisha wanabadilika na kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia na ubunifu, katika kutekeleza majukumu yao ili kuboresha na kutoa huduma bora za afya kwa wananchi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Hassan Khamis Hafidh, amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, kutokana na mageuzi makubwa aliyoyafanya kwenye sekta ya afya hapa Zanzibar.

Naibu huyo alisema kwa sasa Zanzibar imeondokana na changamoto mbali mbali zilizokuwa zinaikabili sekta ya afya, huku maeneo kadhaa muhimu yakimarishwa ikiwemo ICU kwa baadhi ya hospitali Unguja na Pemba.

Amesema huduma nyingi ambazo wananchi wa Zanzibar walikuwa wakizifuata nje, hivi sasa zinapatikana ikiwa ni pamoja na madaktari bingwa kwa baadhi ya maradhi na kukosekana kwa vifaa tiba vya kisasa.

Amefahamisha kuwa kuwa serikali kupitia Wizara ya Afya inaifanyia matengenezo makubwa hospitali ya Mnazi Mmoja, sambamba na kuendelea na mipango ya ujenzi wa hospitali ya Binguni, ambayo itatoa huduma ya matibabu na kutumika kama ni Chuo.

 Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Mngereza Mzee Miraji, amesema lengo la kufanyika kwa kongamano la wiki ya Afya Zanzibar, ni kuielimisha jamii kuhusu afya ya umma, kutambua changamato za mama na mtoto na  kuitangaza Zanzibar kuwa kitovu cha utalii wa tiba.

Dkt. Mngereza amesema katika kongamano hilo programu tatu zilizinduliwa ikiwa ni pamoja na programu ya huduma ya mama na mtoto, programu ya lishe bora na programu ya afya shehia.

Jumla ya wataalamu 4,800 walihudhuria kongamano hilo la wiki ya Afya, ambapo viongozi na watumishi 1973 wamepatiwa mafunzo na elimu ya afya kupitia katika kongamano hilo.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
Tarehe 10.05.2025

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.